1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel inaendelea na mapambano yake dhidi ya Hamas, Gaza

10 Desemba 2023

Wanajeshi wa Israel wamewashambulia wanamgambo wa Hamas Kusini mwa mji wa Gaza wakati Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa akikosoa migawanyiko inayokwamisha majibu ya Baraza lake la Usalama katika mzozo huo.

https://p.dw.com/p/4ZzBw
Israel | Jeshi la Israel
wanajeshi wa Israel wakiwa karibu na mji wa Gaza Picha: Mostafa Alkharouf/Anadolu Agency/picture alliance

Kundi la Hamas linaloongoza Gaza na ambalo mashambulizi yake ya Oktoba 7 kusini mwa Israel yamesababisha mgogoro unaoshuhudiwa sasa kati ya pande hizo mbili, limesema Israel imeushambulia vikali mji wa Khan Yunis na barabara kutoka huko inayoelekea mji wa Rafah unaopakana na Misri.

Israel imesema imelenga maeneo 250 ya wanamgambo hao ndani ya saa 24 zilizopita. 

Nchi za Kiarabu zilishinikiza kukomesha mapigano, huku Umoja wa Ulaya ukiongeza makamanda wawili wa Hamas kwenye orodha yake ya magaidi.

Kulingana na Wizara ya afya ya Gaza, tangu kuanza kwa mashambulizi hayo miezi miwili iliyopita, wapalestina zaidi ya 17,000 wameuwawa wengi wao wakiwa wanawake na watoto. 

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema anasikitishwa na hatua ya kushindwa kwa Baraza la Usalama la Umoja huo, kutoa suluhu ya vita hivyo ikiwa ni siku mbili baada ya Marekani kutumia kura yake ya turufu kupinga azimio la kutaka kusitishwa kwa mapigano hayo.