Israel, Hamas wakaribia makubaliano kuhusu mateka
21 Novemba 2023Kiongozi wa Hamas Ismail Haniyeh amesema kulingana na taarifa iliyotumwa na ofisi yake kwa shirika la habari la AFP, kwamba walikuwa walikaribia kufikia muafaka juu ya mapatano, baada ya Rais wa Marekani Joe Biden, kuashiria kwamba makubaliano yalikuwa karibu jana Jumatatu.
Nchini Qatar, msemaji wa wizara ya mambo ya nje Majed Al-Ansari aliwaambia waandishi habari kwamba wako katika hatua ya karibu zaidi kuwahi kufikiwa ya makubaliano, na kuongeza kuwa wana matumaini makubwa sana.
"Upatanishi umefikia hatua muhimu na ya mwisho na umekwenda mbali zaidi ya masuala ya msingi. Masuala yaliyosalia ni machache, na hii ndiyo karibu zaidi tumefikia kuelekea makubaliano tangu mwanzo wa mzozo huu," alisema Al-Ansar akizungumza na waandishi wa habari mjini Doha.
Soma pia: Hamas yasema makubaliano ya kusitisha vita Gaza yanakaribia
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, ambaye ameapa kuliangamiza vuguvugu la Hamas, amesema ana matumaini kutakuwa na habari njema muda si mrefu, wakati akizungumza na wanajeshi kwenye kambi iliyoko kaskazini mwa nchi hiyo.
Na muda mfupi baada ya hapo, ofisi yake ilitoa taarifa ikisema, kutokana na maendeleo kuhusiana na kuachiwa kwa wafungwa wao, baraza la kivita, baraza la usalama na serikali yatafanya mikutano ya kufuatana Jumanne jioni.
Matumaini ya mafanikio yamekuwa yakiongezeka tangu Qatar iliposema Jumapili kwamba ni masuala madogo tu yamesalia kabla ya kufikia muafaka.
Uvumi uliongezeka zaidi baada ya Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu, ambayo inashiriki mchakato wa kubadilishana wafungwa na kuwaachiliwa kwa mateka, kusema jana Jumatatu, kwamba rais wake alikutana na Haniyeh nchini Qatar.
Mapigano yaendelea kuitikisa Gaza
Licha ya juhudi za kufikia mapatano, mapigano yameendelea kurindima katika vita mbaya zaidi vya Gaza, vilivyosababisha na shambulio la Hamas la Oktoba 7 nchini Israel, ambamo Israel inasema wapiganaji wa kundi hilo waliuawa karibu watu 1,200, wengi wao wakiwa wakiwa raia.
Israel ilijibu shambulio hilo kwa kuanzisha operesheni kali ya mashambulizi ya ndege na ardhini katika Ukanda wa Gaza. Kwa mujibu wa serikali ya Hamas, vita hiyo imesababisha vifo vya zaidi ya watu 13,000, maelfu kati yao wakiwa watoto.
Soma pia: Ujerumani yahimiza uwajibikaji wa kimataifa katika ukanda wa Gaza
Duru za karibu na Hamas na kundi la Islamic Jihad, ambalo pia lilishiriki katika shambulio la Oktoba, zimesema makundi yao yalikubaliana na masharti ya mapatano, ambayo yanajumlisha kipengele cha usitishaji mapigano kwa muda wa siku tano, yanayohusisha usitishaji kamili ya mapigano ya ardhini na kukomesha operesheni ya angani za Israel katika Ukanda wa Gaza, isipokuwa katika eneo la Kaskazini, ambako mapigano yatasimama kwa saa sita tu kila siku.
Chini ya makubaliano hayo, ambayo duru zinasema bado yanaweza kubadilika, kati ya raia 50 na 100 wa Israel pamoja na mateka wa kigeni huenda wakaachiwa, lakini miongoni mwao hakutakuwa na wanajeshi. Na badala yake, Wapalestina wapatao 300 wataachiwa kutoka jela za Israel, miongoni mwao wanawake na watoto.
Wakuu wa mataifa ya BRICS wajadili vita
Wakati hayo yakijiri, viongozi wakuu wa mataifa yanayounda kundi la BRICS - wamekutana kwa njia ya mtandao kujadili mzozo huo na kuhimiza ukomeshaji wa kampeni ya kijeshi ya Israel. Katika mkutano huo ulioitisha na Afrika Kusini, taifa hilo ambalo ndiyo mwenyekiti wa sasa wa BRICS, limeishtumu Israel wa uhalifu wa kivita na "mauaji ya kimbari".
Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa, amesema adhabu ya jumla inayotolewa kwa raia wa Kipalestina kupitia matumizi ya nguvu ya kinyume cha sheria ya Israel ni uhalifu wa kivita, na kuongeza kuwa uzuwiaji wa maksudi wa dawa, mafuta, chakula na maji kwa wakazi wa Gaza ni sawa na mauaji ya kimbari.
Kwa muda mrefu Afrika Kusini imekuwa muungaji mkono mkubwa wa uhuru wa Palestina, huku chama tawala cha ANC kikiihusisha na mpamabano yake dhidi ya utawala wa ubaguzi wa rangi na utengano.
Soma pia:Israel yatangaza kupanua operesheni zake Gaza
Mkutano huo umehudhuriwa kwa njia ya mtandao na viongozi mbalimbali akiwemo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, Rais wa Urusi Vladimir Putin pamoja na viongozi kutoka mataifa ya Saudi Arabia, Argentina, Misri, Ethiopia, Iran na Umoja wa Falme za Kiarabu, ambao wanatazamiwa pia kujiunga na jumuiya hiyo.
Mapema mwezi huu, nchi hiyo iliwarejesha nyumbani wanadiplomasia wake kutoka Israel, na wiki iliyopita iliungana na mataifa mengine kutaka uchunguzi wa mahakama ya kimataifa ya uhalifu, ICC, juu ya mzozo huo.
Siku ya Jumatatu, wizara ya mambo ya nje ya Israel ilimuita nyumbani balozi wake mjini Pretoria kwa mashauriano, wakati ambapo hii leo bunge la Afrika Kusini likijadili muswada wa kuvunja kabisaa uhusiano wa kidiplomasia na Israel.