1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Israel: Benjamin Netanyahu aunda serikali ya mseto

23 Desemba 2022

Waziri mkuu mteule wa Israel Benjamin Netanyahu amefanikiwa kuunda serikali ya mseto kwa kushirikiana na vyama vinavyoelemea mrengo mkali wa kulia.

https://p.dw.com/p/4LMHv
Benjamin Netanjahu
Picha: Abir Sultan/Pool EPA/AP/dpa/picture alliance

Wasiwasi unazidi kuongezeka juu ya serikali hiyo mpya wakati ambapo ghasia zinaongezeka katika eneo la Ukingo wa Magharibi linaokaliwa na Israel. 

Serikali ambayo mwanasiasa huyo mwenye siasa kali ameiunda inatarajiwa kuwa ya mrengo mkali wa kulia isiyokuwa na kifani katika historia ya Israel. Imesababisha hofu ya kuendelea kwa mivutano ya kijeshi kwenye Ukingo wa Magharibi katika muktadha wa kiwango kikubwa cha umwagikaji wa damu bila ya kifani katika miaka 20 iliyopita.

Soma Pia:Waisraeli wanapiga kura

Chama cha Netanyahu cha Likud kimepewa jukumu la kuunda serikali baada ya uchaguzi wa mwezi Novemba kwa kuungwa mkono na vyama hivyo yenye itikadi kali pamoja na vyama vya mrengo mkali wa kulia. Watakao kuwa na sauti kubwa kwenye serikali hiyo mpya ya mseto ni pamoja na Bezalel Smotrich na Itamar Ben Gvir ambao ni viongozi wa kambi ya kizayuni wanaofuata itikadi kali ya mrengo wa kulia.

Chama cha Likud kilihitaji washirika kuunda serikali ya mseto.

Kushoto: Waziri Mkuu mteule wa Israel Benjamin Netanyahu. Kulia: Rais wa Israel Isaac Herzog.
Kushoto: Waziri Mkuu mteule wa Israel Benjamin Netanyahu. Kulia: Rais wa Israel Isaac Herzog.Picha: Maya Alleruzzo/AP/picture alliance

Netanyahu, kiongozi wa chama cha kihafidhina cha Likud alimfahamisha Rais wa Israel Isaac Herzog juu ya kuunda serikali yake mpya jana Jumatano jioni muda mfupi kabla ya kumalizika muda wa kuunda serikali mpya itakayotawala nchini humo.

Benjamin Netanyahu, aliyekuwa waziri mkuu wa Israel kutoka mwaka 1996 hadi 1999 na kisha kurudi tena mamlakani tena kutoka mwaka 2009 hadi 2021, katika uchaguzi uliomalizika aliongoza chama chake cha Likud kuchukua wingi wa viti  bungeni katika uchaguzi wa tano nchini humo ndani ya kipindi cha miaka minne. Hata hivyo, kwa viti 32 pekee, chama cha Likud kilihitaji washirika kuunda serikali ya mseto ili kupata jumla ya viti 61 katika bunge la Israel, Knesset.

Hatua hiyo ya kuundwa serikali mya ya Israel ni baada ya wiki kadhaa za mazungumzo magumu kati ya chama cha Likud na washirika wake ambao bado mpaka sasa hawajakamilisha mikataba ya kugawana madaraka na Chama cha Likud cha Netanyahu. Hata hivyo, Netanyahu amesema anakusudia kukamilisha mchakato huo wiki ijayo ingawa tarehe kamili haikutajwa.

Soma Pia:Netanyahu aongezewa muda kuunda serikali mpya

Hata akifanikiwa, Netanyahu anakabiliwa na kazi ngumu siku za usoni. Inahofiwa muungano wake na vyama vya itikadi kali za kidini utaleta mabadiliko makubwa ambayo yanaweza kuwagawanya watu wa Israeli, kuongezeka migogoro na Wapalestina na pia kuiweka Israel kwenye mkondo wa mgongano na baadhi ya washirika wake wa karibu, ikiwa ni pamoja na Marekani na jumuiya ya Wayahudi ya Marekani.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken amempongeza Benjamin Netanyahu kwa kuunda serikali, ambayo inajumuisha vyama vya siasa kali za mrengo wa kulia, na ametoa wito wa kujitolea na kuzingatia maadili ikiwa ni pamoja na haki za Wapalestina.

Vyanzo: AP/DPA/AFP