IS yazidi kupigana licha ya mashambulizi dhidi yake
28 Oktoba 2014Maafisa wa jeshi la Marekani wamesema kuwa wamefanya mashambulizi saba ya anga dhidi ya kundi la IS kati ya Jumapili na jana Jumatatu. Mashambulizi hayo yalijikita nchini Irak, yakilenga ngome za kundi hilo karibu na bwawa la Mosul na katika maeneo ya mji Fallujah ulio kusini mashariki.
Msemaji wa wizara ya ulinzi ya Marekani Bill Urban amesema mashambulizi haya dhidi ya IS ambayo yalianza Agosti mwaka huu yameigharibu nchi hiyo kitita cha dola milioni 580. Kwa ujumla ndege za Marekani na za washirika wake zimefanya mashambulizi 6,600 dhidi ya IS.
Awali wizara ya ulinzi ya Marekani ilikuwa imesema mashambulizi hayo yanaigharimu dola milioni 7 kwa siku, lakini wachambuzi wa kujitegemea wamesema makadirio hayo ni ya chini.
Mkutano kuhusu wakimbizi wa Syria
Wakati hayo yakijiri Mashariki ya Kati, katika mji mkuu wa Ujerumani- Berlin leo umeanza mkutano wa kuzungumzia suala la wakimbizi wa vita vinavyoendelea nchini Syria. Wawakilishi wa nchi 40 zinazoshiriki katika mkutano huo, wanatafuta jibu kwa changamoto zitokanazo na upungufu wa msaada wa kibinadamu kuwasaidia wahanga wa vita hivyo.
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier amesema kinachohitajika ni kuimarisha mkakati uliopo.
‘‘Hatuna haja ya kubadilisha mtazamo, bali kuimarisha mikakati iliyopo. Hatupaswi tu kuishia katika kuwashughulikia wakimbizi, tunalazimika pia kujihusisha na utangamano wa nchi zinazowapokea wakimbizi hao‘‘. Amesema Steinmeier.
Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwashughulikia wakimbizi UNHCR linakadiria kuwa watu milioni 3 wamekimbia kutoka Syria na kuhamia mataifa jirani, huku wengine zaidi ya milioni 6.5 wakiwa wakimbizi wa ndani ya nchi.
Hakuna msaada kwa wakurdi wa Syria
Nchini Syria kwenyewe mapigano makali yameendelea karibu na mji muhimu wa Kobane ulio karibu na mpaka kati ya Syria na Uturuki. Mwandishi wa shirika la AFP aliye karibu na mji huo amesema wapiganaji wa kikurdi wamekuwa wakipigana kufa na kupona kuwazuia wanamgambo wa IS kusonga mbele wakiukaribia mji huo.
Bado hakuna dalili zozote za msaada ulioahidiwa kwa wakurdi hao; ahadi kwamba wanajeshi wa mamlaka ya wakurdi wa Irak wajulikanao kama Peshmerga wangewasili na zana nziti za kijeshi kuwasaidia wenzao wa Syria bado haijatimizwa. Afisa wa kikurdi amesema msaada huo umekwamishwa na Uturuki, ambayo ilikuwa imekubali kuwapa njia wanajeshi hao.
Mwandishi: Daniel Gakuba/AFPE/ DW website
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman