1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ndege za washirika zinaendelea na mashambulizi ya anga

9 Oktoba 2015

Licha ya mashambulizi ya anga yanayofanywa na vikosi vya kimataifa dhidi yake, kundi la IS limesonga mbele jimboni Aleppo na kukamata miji na vijiji kadhaa vilivyokuwa chini ya udhibiti wa makundi mengine ya waasi.

https://p.dw.com/p/1GlZE
Waasi wa IS wameteka maeneo mapya licha ya kuandamwa na mashambulizi ya anga
Waasi wa IS wameteka maeneo mapya licha ya kuandamwa na mashambulizi ya angaPicha: Colourbox/krbfss

Kwa mujibu wa shirika linalochunguza haki za binadamu nchini Syria lenye makao nchini Uingereza, kuyateka maeneo hayo karibu na Aleppo ndio hatua kubwa iliyopigwa na kundi la IS kwenye uwanja wa mapambano katika muda wa miezi kadhaa. Mkuu wa shirika hilo Rami Abdel Rahman amesema kulikuwa na mashambulizi makali ya anga katika maeneo hayo mapya yaliyotekwa na IS.

Ushirika wa kijeshi unaoongozwa na Marekani umekuwa ukiendesha operesheni ya anga dhidi ya kundi hilo kwa zaidi ya mwaka sasa, na Urusi imetangaza hivi karibuni kuanza kulishambulia kundi hilo, ingawa azma ya nchi hiyo inaonekana kuwa kumuunga mkono mshirika wake rais Bashar al-Assad, katika vita vyake dhidi ya waasi, katika juhudi za kulikomboa eneo la pwani lililo magharibi mwa nchi. Urusi inacho kituo cha jeshi lake la majini katika eneo hilo.

Ufaransa yashambulia ''kambi ya magaidi'' Raqqa

Wakati huo huo waziri wa ulinzi wa Ufaransa Jean Yves Le Drian amesema jeshi la nchi hiyo limekishambulia kituo cha IS katika mji wa Raqqa, ambao amedai kilikuwa kikitumiwa kuwapa mafunzo magaidi ambao ni tishio kwa Ulaya.

Jean Yves le Drian, waziri wa ulinzi wa Ufaransa
Jean Yves le Drian, waziri wa ulinzi wa UfaransaPicha: AFP/Getty Images/N. Tucat

''Ufaransa imefanya mashambulizi nchini Syria usiku huu.Tumefanya mashambulizi hayo kwa sababu tunafahamu kwamba nchini humo hususan katika maeneo ya Raqqa, kipo kituo cha mafunzo kwa ajili ya wapiganaji wa kigeni, ambao hawatayarishwi kupigana upande wa IS ndani ya Syria, bali wanaandaliwa kuja Ufaransa, na Ulaya kufanya mashambulizi''. Amesema waziri le Drian.

Hayo yanaarifiwa wakati kukiwa na taarifa zilizotolewa na shirika la habari la Iran, Fars ambazo zimeeleza kwamba Jenerali kikosi cha ulinzi wa mampinduzi cha nchi hiyo, Hussein Hamedani ameuawa nchini Syria. Shirika jingine la habari la al-Mayadeen la nchini Lebanon ambalo linaegemea upande wa Iran, limesema jenerali huo amekufa mjini Aleppo.

Kazi pevu kwa waasi wa Syria

Makundi kadhaa ya waasi wa Syria yalio katika mji wa Aleppo, yakiwemo yale yenye msimamo mkali wa kiislamu, yamejikuta yakipigana na maadui wawili, yaani serikali ya rais Bashar al-Assad na Dola la Kiislamu, IS.

Makundi hayo hutegemea udhibiti wao wa kaskazini mwa jimbo la Aleppo ambako kuna njia muhimu inayowapitishia msaada. Uturuki ambayo inayaunga mkono makundi hayo ya waasi wa Syria, inahofia kwamba huenda IS ikalikamata eneo lenye barabara muhimu kwenye mpaka baina yake na Syria katika mkoa huo wa Aleppo. Waasi hao wamefanikiwa kuuteka mkoa wa Idlib kutoka mikononi mwa serikali ya rais Assad, lakini sasa wanakabiliwa na mashambulizi ya anga ya ndege za Urusi.

Uturuki imesema leo hii kwamba ina wasi wasi mkubwa kutokana na wimbi jipya la wakimbizi wa Syria, ambao imesema limesababishwa na mashambulizi ya Urusi.

Mwandishi: Daniel Gakuba/dpae/afpe

Mhariri:Saumu Mwasimba