IS yaliharibu hekalu mjini Palmyra
24 Agosti 2015Mji wa Palmyra unaofahamika sana kutokana na magofu ya Himaya ya Kiroma yaliyohifadhiwa vizuri, ulikamatwa na wapiganaji wa IS kutoka kwa majeshi ya serikali mwezi Mei, na kuzusha hofu kuwa wanagambo hao huenda wakaharibu turathi zake kama tu walivyofanya katika maeneo mengine ya Syria na Iraq.
Hadi kufikia jana, maeneo mengi maarufu mjini Palmyra yalikuwa katika hali nzuri, ijapokuwa kulikuwa na ripoti kuwa IS iliyapora na kudaiwa kuharibu sanamu ya samba nje ya jumba la makumbusho la mji huo.
Shirika la Haki za Binaadamu la Syria, lenye makao yake nchini Uingereza ambalo hufuatilia vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria, limethibitisha kuharibiwa kwa hekalu la Baal Shamin
IS ambayo inadhibiti maeneo makubwa ya Syria na nchi jirani Iraq, iliukamata mji wa Palmyra mnamo Mei 21, na kuzusha wasiwasi kutoka kwa jamii ya kimataifa kuhusu hatima ya eneo hilo la turathi linalotajwa na Shirika la UNESCO kuwa “lenye thamani kubwa ulimwenguni”.
Kabla ya kuzuka mgogoro wa Syria mnamo Machi 2011, zaidi ya watalii 150,000 walizuru Palmyra kila mwaka, wakivutiwa na sanamu za kupendeza, zaidi ya nguzo 1,000. IS ililichimba eneo hilo la kale mwezi Juni kabla ya kuharibu Sanamu ya Simba maarufu kama Athena – sanamu ya kipekee iliyotengenezwa kwa mawe ya chokaa yenye urefu wa mita 3 nje ya jumba la makumbusho.
Vitu vingi vya kale katika jumba hilo la makumbusho vilihamishwa na wafanyakazi wa mambo ya kale kabla ya IS kuwasili, ijapokuwa kundi hilo limeyalipua makaburi kadhaa ya kihistoria ya kiislamu.
Matukio haya ya karibuni yamekuja siku chache tu baada ya wapiganaji wa jihadi wa IS kumchinja mtalaamu mkuu wa mambo ya kale wa mji wa Palmyra aliyekuwa na umri wa miaka 82. IS pia iliwaua mamia ya watu mjini humo na viunga vyake, wengi wao wafanyakazi wa serikali, na kuwatumia wanachama wao watoto kuwapiga risasi na kuwauwa wanajeshi 25 wa serikali ya Syria katika ukumbi wa kale wa sanaa wa mjini Palmyra.
Katika nchi jirani Iraq, ambako IS pia inadhibiti eneo kubwa la nchi hiyo, kundi hilo la jihadi liliteketeza kabisa vitu vya eneo la kale la Mesopotamia na kuiba vitu vingine ili kuuza katika soko la magendo.
Mwezi Februari, walitoa mkanda wa video ukionyesha wanamgambo hao wakitumia sululu kuharibu sanamu katika mji wa pili kwa ukubwa nchini humo Mosul. Kundi hilo pia limechoma moto maelfu ya vitabu na nakala za kale.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Iddi Ssessanga