1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iraq kumuita balozi wa Iran kupinga mashambulizi

28 Septemba 2022

Serikali ya Iraq imesema itamuita balozi wa Iran mjini Baghdad kupinga mashambulizi ya makombora ya ndege zisizo na rubani yaliyofanywa na Iran dhidi ya jimbo la kaskazini mwa Iraq la Kurdistan

https://p.dw.com/p/4HTWb
Irak | Präsident Barham Salih
Picha: Murtadha Al-Sudani/AA/picture alliance

Katika taarifa, msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Iraq Ahmed al-Sahaf amesema kuwa balozi huyo wa Iran nchini Iraq ataitwa haraka kupewa barua ya malalamiko kuhusu mashambulizi dhidi ya jimbo lenye utawala wa ndani la Kurdistan, Kaskazini mwa Iraq . Wizara ya afya katika eneo hilo la Kurdstan imesema mashambulizi ya ndege zisizo na rubani za Iran yaliyozilenga kambi za kundi la upinzani la Wakurdi wa Iran wanaoishi Kaskazini mwa Iraq imesababisha vifo vya watu wasiopungua tisa na kuwajeruhi wengine 32.

Maandamano yaendelea kushuhudiwa Iran

Mashambulizi hayo yalifanyika huku maandamano yakiendelea kushuhudiwa katika taifa hilo la Kiislamu baada ya kifo cha Mahsa Amini, aliyepoteza maisha akiwa chini ya kizuizi cha polisi wa maadili nchini Iran.

Soran Nuri, mwanachama wa chama cha Demokrasia cha Wakurdistan nchini Iran, amesema mashambulizi ya Iran yalilenga eneo la Koya lililoko umbali wa kilomita 65 Mashariki mwa Irbil, ambao ni mji mkuu wa jimbo la Wakurdi. Kundi hilo linalojulikana kwa kifupi kama KDPI, ni kundi la mrengo wa kushoto wa kikosi cha upinzani lililopigwa marufuku nchini Iran.

Wizara ya mambo ya nje ya Iraq pamoja na serikali ya kikanda ya Kurdistan, zimelaani mashambulizi hayo.

Ayatollah Ali Khamenei
Kiongozi mkuu wa Iran Ayatollah Ali KhameneiPicha: IRANIAN LEADER PRESS OFFICE/AA/picture alliance

Huku hayo yakijiri, polisi wa kukabiliana na ghasia nchini Iran Jumatano walipelekwa katika viwanja mbalimbali nchini humo kukabiliana na waandamanaji waliokuwa wakipaza sauti kulaani kifo cha Mahsa Amini huku maandamano ya kote nchini humo kuhusiana na kifo cha Amini yakiweka shinikizo kwa mamlaka za Dola hiyo ya Uajemi.

Wairani watoa wito wa kumalizika kwa taasisi za Kiislamu

Licha ya kuongezeka kwa idadi ya vifo na ukandamizaji unaofanywa na vikosi vya usalama vinavyotumia gesi ya kutoa machozi, virungu na wakati mwingine risasi za moto, video zilizotumwa kwenye mitandao ya kijamii zimeonesha Wairani wakitoa wito wa kumalizika kwa taasisi za Kiislamu zaidi ya miongo minne madarakani.

Maandamano yameendelea kwa takriban wiki mbili na kuenea katika miji 80 kutoka Tehran hadi Kusini Mashariki mwa bandari ya Chabahar. Video kutoka Chabahar, imeonesha polisi wakukabiliana na ghasia wakifyetua gesi za kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji waliokuwa wakiimba ''kifo kwa kiongozi mkuu Ayatollah Ali Khamenei.'' Vyombo vya habari vya serikali vimesema watu 41 wakiwemo maafisa wa polisi na wapiganaji wanaoiunga mkono serikali, wamekufa wakati wa maandamano hayo huku mashirika ya kutetea haki za binadamu nchini Iran yakiripoti idadi kubwa zaidi.

 

.