Iran yautaka Umoja wa Ulaya kukomesha tabia ya kutowajibika
29 Novemba 2024Iran leo imetoa wito kwa Umoja wa Ulaya kubadili mwenendo wake kwa nchi hiyo, baada ya mazungumzo na mwanadiplomasia mkuu wa Umoja huo wa Ulaya Enrique Mora mjini Geneva nchini Uswisi.
Katika taarifa iliyochapishwa katika mtandao wa kijamii wa X baada ya ujumbe wa Iran kufanya mazungumzo na Mora, naibu waziri wa mambo ya nje wa Iran Kazem Gharibabadi, amesema ilithibitishwa tena kwa Mora kwamba Umoja wa Ulaya unapaswa kuacha tabia yake aliyoitaja kuwa ya ubinafsi na kutowajibika kwa maswala na changamoto za bara hilo na mambo ya kimataifa.
Hii leo, Uingereza, Ufaransa na Ujerumanizinatarajiwa kufanya mazungumzo na ujumbe wa Iran kuhusu mpango wa nyuklia wa nchi hiyo.
Wakati huo huo, ripoti ya shirika la nyuklia la Umoja wa Mataifa imethibitisha kuwa Iran inapanga kuweka takriban mashine 6,000 za kurutubisha madini ya urani.