Iran yasema haitishiki kwa kauli za Trump
23 Julai 2018Iran imesema vitisho vya Rais Donald Trump dhidi ya Jamhuri hiyo ya kiislamu ni sawa na mapambano ya kisaikolojia, na Iran itaendelea kupambana na maadui zake. Iran imekasirishwa na Marekani kufuatia pia hotuba iliyotolewa jana na waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo aliyewatuhumu viongozi wa jamhuri hiyo kuwa ni mafia.
Katika hotuba ya Pompeo jumapili aliwalaani viongozi wa Iran na kuwaita ni mafia na kuahidi kwamba Marekani itachukua hatua ambazo hazikutajwa,kuwaunga mkono Wairan ambao hawaridhishwi na viongozi wao.
''Wakati mwingine inaonekana kama dunia imeunyamazia uimla unaofanyika Iran na kampeini zake za vurugu nje ya nchi.Lakini watu wa Iran wenye mapenzi na nchi yao hawakai kimya kuhusu ukiukaji mkubwa unaofanywa na serikali ya nchi yao na Marekani chini ya rais Trump pia haitokaa kimya.Kwa kuangazia upinzani wa haya na miaka 40 ya utawala wa kibabe,nina ujumbe kwa watu wa Iran,Marekani inawasikia,Marekani inawaunga mkono.Marekani iko pamoja nanyi.Marekani inapoona nguvu za uhuru zinaangamizwa tunaahidi mshikamano.''
Hotuba ya Pompeo imekosolewa vikali nchini Iran ambapo Jamhuri hiyo ya kiislamu imesema kauli iliyotolewa na waziri huyo wa mambo ya nje wa Marekani kuhusu viongozi wake ni kuingilia kati masuala ya ndani ya nchi hiyo. Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Iran Bahram Qasemi amesema hotuba hiyo imeonesha uingilia kati wa wazi wa Marekani katika masuala ya nchi ya Iran na sera kama hizo zitawaunganisha wairan ambao watazishinda njama za kutaka kuihujumu nchi hiyo.Wachambuzi wa Iran wamepuuza kitisho cha Trump na serikali ya Marekani kwa ujumla. Mwandishi wa Iran Mohsem Taheri anasema vitisho vya serikali ya Marekani dhidi ya Iran vimeanza muda mrefu lakini sasa vinavuka mpaka.
Kwa miaka mingi,Marekani na Iran zimekuwa zikitoleana vitisho kwa njia mbali mbali.Malumbano ya vita vya maneno ni asili ya Trump.Nadhani tusimpe sababu na kumfanya apate nafasi kubwa kadri iwezekanavyo ili watu waepuke kuingia katika vita au kitu kama hicho.
Rais wa Iran Hassan Rouhani alisema sera za chuki za rais Trump kuelekea Iran huenda zikasababisha vita vikubwa kabisa ambavyo havijapata kuonekana na Trump nae akajibu usiku ujumbe huo kupitia Twita na kuandika kwa herufi kubwa akimwambia Rouhani asijaribu hata siku moja katika maisha yake kuitishia Marekani la sivyo atakabiliana na athari zake. Maafisa wa Marekani wanaolifahamu kwa kina suala hili la kutupiana maneno ya vitisho,kwa upande wa Marekani wanasema ni hatua inayokusudiwa kwenda sambamba na kutia msukumo wa kuwekwa vikwazo na kusaidia katika kuishinikiza Iran kusitisha mpango wake wa Nyuklia pamoja na hatua ya kuunga mkono makundi ya wanamgambo.
Mwandishi: Saumu Mwasimba
Mhariri: Iddi Ssessanga