1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yasema haina matumaini katika mazungumzo ya Vienna

Zainab Aziz Mhariri: Iddi Ssessanga
11 Februari 2022

Rais wa Iran Ebrahim Raisi amesema nchi yake haina matumaini sana juu ya mazungumzo yanayoendelea ya mjini Vienna juu ya kuyafufua makubaliano ya nyuklia ya mwaka 2015 kati ya nchi hiyo na nchi zenye nguvu duniani.

https://p.dw.com/p/46tJ6
Russland Treffen Putin und Raisi Präsident Iran
Picha: Pavel Bednyakov/SPUTNIK/REUTERS

Iran na Marekani zilianza tena mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kwenye mji mkuu wa Austria, Vienna mnamo siku ya Jumanne baada ya mapumziko ya siku 10, lakini wajumbe kwenye mazungumzo hayo hawajafahamisha bado iwapo wanakaribia kusuluhisha masuala mbalimbali yaliyochomoza.

Mjumbe wa Iran Ali Bagheri Kani katika mazungumzo ya nyuklia ya mjini Vienna, Austria
Mjumbe wa Iran Ali Bagheri Kani katika mazungumzo ya nyuklia ya mjini Vienna, Austria.Picha: Guo Chen/Xinhua/picture alliance

Rais wa Iran amesema nchi yake haina matumaini yoyote katika mazungumzo hayo ya Vienna na kwamba Iran itaendelea kutegemea uwezo wa uchumi wake wa ndani badala ya kutarajia msaada kutoka ng'ambo na suluhisho litakalotokana na mazungumzo ya nyuklia kati ya Iran na mataifa yenye nguvu duniani.

Soma Zaidi:Marekani na Iran zahimizwa kurejelea makubaliano ya nyuklia

Kiongozi huyo Ibrahim Raisi amesema Iran iamtumainia Mungu, pia ina matumaini makubwa katika maeneo ya Khuzestan, Khorasan, Azerbaijan katika maeneo ya mashariki, magharibi, kaskazini na kusini mwa nchi hiyo. Amesema Iran kamwe haina matumaini yoyote na Vienna au New York.

Utawala wa Rais wa Marekani Joe Biden uliishinikiza hadharani Iran siku ya Jumatano juu ya kufikia makubaliano haraka, kwa kusema haitawezekana kurudi kwenye makubaliano ya nyuklia iwapo mazungumzo ya mjini Vienna hayatafikia makubaliano katika wiki za hivi karibuni. Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergei Lavrov amesema safari bado ni ndefu kabla ya mapatano mapya kufikiwa kati ya Marekani na Iran.

Wajumbe wa Umoja wa Ulaya, Iran na wengineo kwenye mazungumzo ya nyuklia ya mjini Vienna.
Wajumbe wa Umoja wa Ulaya, Iran na wengineo kwenye mazungumzo ya nyuklia ya mjini Vienna.Picha: Askin Kiyagan/AA/picture alliance

Wizara ya mambo ya nje ya Iran imesema Marekani inapaswa kufanya maamuzi ya kisiasa kuhusu kuondoa vikwazo kama Iran ilivyotaka, imesemya vikwazo hivyo viondolewe kikamilifu ndipo mkataba wa mwaka 2015 uweze kufufuliwa na kwamba hilo halina mjadala.Mazungumzo ya nyuklia na Iran kuendelea Vienna.

Soma Zaidi: Mazungumzo ya nyuklia na Iran kuendelea Vienna

Rais wa hapo awali wa Marekani Donald Trump aliiondoa nchi yake kwenye mkataba wa nyuklia na Iran mnamo mwaka 2018. Mkataba huo ulihusu kuizuia Iran kuunda silaha za nyuklia. Badala yake Trump alirejesha vikwazo dhidi ya Iran ili kuilazimisha nchi hiyo irudi kwenye meza ya mazungumzo kujadili mkataba mwingine ambao pia ungelihusisha mpango wake wa makombora ya mafasa marefu na misaada inayotoa  kwa mawakala wake katika mashariki ya kati. Iran ilijibu kwa kukiuka vipengee vingi vya mkataba na kuchukua hatua ndefu zaidi za kurutubisha madini ya Urani kiasi cha kukaribia hatua ya kuunda bomu la nyuklia.

Chanzo:RTRE