1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Migogoro

Iran yapuuza miito ya Ulaya ya kutoishambulia Israel

13 Agosti 2024

Wizara ya mambo ya nchi za nje ya Iran leo, imesema miito ya Ujerumani, Ufaransa na Uingereza ya kuitaka Iran isifanye mashambulizi ya kulipiza kisasi dhidi ya Israel, "haina mashiko ya kisiasa."

https://p.dw.com/p/4jPAS
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Iran Nasser Kanaani
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Iran Nasser Kanaani Picha: Iranian Foreign Ministry/Zuma/picture alliance

Wizara ya mambo ya nchi za nje ya Iran leo, imesema miito ya Ujerumani, Ufaransa na Uingereza ya kuitaka Iran isifanye mashambulizi ya kulipiza kisasi dhidi ya Israel, "haina mashiko ya kisiasa na inakwenda kinyume na maadili ya sheria ya kimataifa."

Msemaji wa wizara hiyo ya mambo ya nje ya Iran Nasser Kanaani amesema, Tehran imedhamiria kuyasimamisha mashambulizi ya Israel na kuzitaka Ujerumani, Ufaransa na Uingereza kusimama na kuvipinga vita vya Israel dhidi ya Hamas huko Gaza na hatua ya Israel ya kutoa kauli za kuchochea vita hivyo.

Nchi hizo tatu za Ulayahapo jana Jumatatu, zilitoa taarifa ya pamoja ya kuitaka Iran na wandani wake kusita kuishambulia Israel, kufuatia mauaji ya mkuu wa kisiasa wa hamas, Ismael Haniyeh mwezi uliopita mjini Tehran. Iran na wandani wake Hamas na kundi la wanamgambo wa Kishia la Hezbollah huko Lebanon, wameituhumu Israel kwa kufanya mauaji hayo. Israel haijatoa kauli yoyote ya kudai kuhusika.