1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yaondoa kamera za IAEA kwenye vinu vyake

Josephat Charo
9 Juni 2022

Shirika la Kimataifa la kudhibiti silaha za nyuklia IAEA limetahadharisha juu ya pigo kubwa dhidi ya mkataba wa nyuklia kati ya nchi za Magharibi na Iran,huku Iran ikiondoa kamera 27 katika vinu vyake ya nyuklia.

https://p.dw.com/p/4CUTu
Österreich Sitzung IAEA-Gouverneursrat
Picha: Askin Kiyagan/AA/picture alliance

Mkurugenzi mkuu wa shirika la IAEA Rafael Grossi anasema Iran inaondoa kamera 27 zilizowekwa katika vinu vya nishati ya nyuklia, kikiwemo kinu cha chini ya ardhi cha Natanz, kinachotumiwa kurutubisha madini ya urani, pamoja na kinu cha Isfahan. Akizungumza kwenye mkutano na waandishi habari mjini Vienna, Austria, Grossi amesema hatua hiyo inaongeza kitisho cha wachunguzi wake kutoweza kufuatilia shughuli za mpango wa nyuklia wa Iran huku inapoendelea na urutubishaji wa madini ya urani kufikia viwango vya kutengeneza silaha.

"Kimsingi tulichofahamishwa ni kwamba kamera 27 zinaondolewa na Iran mbali na mfumo wa mtandaoni wa ufuatiliaji urutubishaji tulio nao huko. Kwa hiyo hii bila shaka ni changamoto kubwa kwa uwezo wetu wa kuendeea kufanya kazi huko na kuthibitisha uhakiki wa tangazao la Iran chini ya mkataba wa nyuklia wa mwaka 2005 wa JCPOA."

Grossi pia ametahadharisha kwamba hatua ya Iran kuondoa kamera itakuwa pigo kubwa kwa mazungumzo kuhusu mkataba wa nyuklia kati ya Iran na mataifa ya magharibi. Mkurugenzi huyo raia wa Argentina, amesema kamera kiasi 40 zitaendekea kufanya kazi na sasa wako katika hali ya wasiwasi.

Iran haijatoa kauli yoyote kuthibitisha inaondoa kamera hizo, ingawa ilitishia siku ya Jumatano itachukua hatua zaidi kufuatia mzozo wa mwaka mmoja unaotishia kutanua mashambulizi zaidi katika eneo lote la Mashariki ya Kati.

Naftali Bennett
Waziri Mkuu wa Israel, Naftali BennettPicha: Tsafrir Abayov/Pool/picture alliance

Bennett kujadili suala la Iran Abu Dhabi

Mpango wa nyuklia wa Iran unatarajiwa kupewa kipaumbele kikubwa katika ajenda ya mazungumzo katika ziara ya Waziri Mkuu wa Israel, Naftali Bennett, katika Umoja wa Falme za Kiarabu, ambako anatarajiwa kukutana na mwanamfalme Mohamed bin Zayed kujadiliana juu ya masuala ya kikanda. Kabla kuondoka Israel Bennett alizisifu nchi zinazokutana kwenye mkutano wa shirika la IAEA mjini Vienna zilizopiga kura kuibana Iran kuwa wazi zaidi kuhusiana na shughuli zake za nyuklia katika vinu vitatu ambavyo haijavitangaza nchini humo.

"Naipongeza IAEA kwa uamuzi wake uliopitishwa na bodi ya magavana, uamuzi unaoonesha wazi kwamba Iran inaendelea kufanya ujanja, kuficha na kutotoa tarifa. Tunaona katika uamuzi huu uongo na unafiki wa Iran kwa upande mmoja, na kwa ujumla kwa upande mwingine tunaona msimamo sahihi wa nchi za dunia katika kutofautisha mema na mabaya, wanaposema Iran inaficha mambo. Hatutaliachia jambo hili."

Uamuzi wa Iran unafuatia hatua iliyochukuliwa na bodi ya magavana wa IAEA kushinikiza Jamhuri ya kiislamu ya Iran kutoa taarifa za kuaminika kuhusu nyenzo za nyuklia zilizotengenezwa na binadamu ziizopatikana katika vitu vyake vitatu.

Awali Grossi aliwafahamisha wanachama wa IAEA kwamba Iran ililifahamisha shirika hilo kuwa inapanga kufunga mitambo miwili aina ya IR-6 katika kinu chake cha Natanz, ambayo inatumika kuharakisha urutubishaji wa gesi ya urani mara kumi zaidi kuliko mfumo wa awali na nyenzo ambazo ililazimika kutumia chini ya mkataba wa nyuklia na nchi za magharibi.

(ape, reuters, dpa)