Iran yamnyonga mtu wa pili kuhusiana na maandamano
12 Desemba 2022Kulingana na taarifa iliyochapishwa na mtandao wa shirika la habari za mahakama nchini Iran, Mizan, Majidreza Rahnavard alinyongwa hadharani leo Jumatatu katikati ya mji badala ya gerezani.
Taarifa hiyo imesema Rahnavard (ambaye umri wake haujabainika vyema) alihukumiwa kifo na mahakama ya mji wa Mashhad, kwa kuwaua maafisa wawili wa usalama kwa kutumia kisu, na kuwajeruhi watu wengine wanne.
Tukio hilo la kunyongwa kwa Rahnavard limezusha ghadhabu zaidi ulimwenguni. Mnamo Alhamisi wiki iliyopita taifa hilo la Kiislamu lilimnyonga mtu mwengine Mohsen Shekari aliyekuwa na umri wa miaka 23.
Tukio la kwanza la unyongaji kuhusiana na maandamano
Shekari pia alinyongwa kwa kosa la kumshambulia afisa wa usalama wakati wa maandamano. Tukio hilo vilevile lilizusha ghadhabu la lililaaniwa vikali na Ulaya na Marekani.
Mwishoni mwa wiki, makundi ya kutetea haki za binadamu yalitahadharisha kwamba watu wengine waliokamatwa kuhusiana na maandamano nchini Iran wapo katika hatari kubwa ya kunyongwa.
Iran yamkamata naibu mhariri wa shirika la habari la Fars
Maandamano hayo yalichochewa na kifo cha msichana mwenye umri wa miaka 22 Mahsa Amini mikononi mwa polisi wa maadili kwa madai ya kutovaa Hijab hivyo kukiuka sheria kuhusu namna wanawake wanavyopaswa kuvaa nchini humo.
Maandamano hayo ambayo mamlaka za usalama zimetaja kuwa vurugu, ni changamoto kubwa kwa serikali tangu mapinduzi ya mwaka 1979 nchini humo. Waandamanaji wamekabiliwa na ukandamizaji ambao wanaharakati wanasema unalenga kuwatia wananchi hofu.
Hukumu za kifo mahakamani
Kabla ya visa viwili vya unyongaji ambavyo tayari vimetekelezwa, mahakama ya Iran ilisema watu 11 wamehukumiwa kifo kuhusiana na maandamano hayo. Lakini watetezi wa haki za binadamu wamesema zaidi ya wengine 12 pia wanakabiliwa na mashtaka ambayo huenda adhabu ikawa ni kifo.
Iran yatoa hukumu ya kifo kwa waandamanaji
Baada ya kisa cha leo, Omid Memarian ambaye ni mchambuzi katika kituo cha Democracy for the Arab World Now (DAWN) yaani Demokrasia kwa Ulimwengu wa Kiarabu Sasa, amesema kesi hizo zinaendeshwa bila kufuata taratibu stahiki na si za haki. Amesema hivyo ndivyo serikali inataka kuyazima maandamano hayo ya nchi nzima.
Masih Alinejad, raia wa Iran aliyeko uhamishoni Marekani, amesema Majidreza Rahnavard ameuawa kwa sababu ya kupinga kuuawa kwa Mahsa Amini, serikali imeamua kuwanyonga waandamanaji. Amezitaka nchi za Umoja wa Ulaya kuwatoa mabalozi wao nchini Iran.
Shutuma za kimataifa
Wiki iliyopita baada ya tukio la kwanza la unyongaji, waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Annalena Baerbock alisema kitendo hicho kinaonesha dharau isiyo na kikomo kwa maisha ya binadamu.
1,000 washitakiwa kwa kuandamana Iran
Nchi nyingine ambazo zililaani kitendo hicho cha Iran ni pamoja na Uingereza, Canada na Umoja wa Mataifa.
Kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa, zaidi ya waandamanaji 14,000 wametiwa nguvuni nchini Iran.
(AFPE)
Tafsiri: John Juma
Mhariri: Yusuf Saumu