Mamia wajitokeza kuwazika waliouawa kwenye milipuko Iran
5 Januari 2024Mazishi hayo ya Ijumaa yamefanyika katika msikiti wa Emam Ali huko mjini Kerman ambako umati wa waombolezaji ulikusanyika mbele ya majeneza yaliyozungushwa bendera za Iran. Umati huo wa waombolezaji ulisikika ukiimba maneno ya "kisasi! Kisasi!" kwenye mji wa Kerman, kulitokea milipuko miwili siku ya Jumatano ambayo imetajwa kuwa shambulio baya nchini Iran tangu mapinduzi ya Kiislamu ya mwaka 1979.
Rais wa Iran Ebrahim Raisi na kamanda mkuu wa jeshi la mapinduzi Hossein Salami, wote wameapa kulipiza kisasi dhidi ya mashambulizi hayo ambayo yanadaiwa kufanywa na kundi linalojiita na Dola la Kiislamu IS.
Shirika la habari la Iran IRNA limemnukuu Rais Ebrahim ambaye pia alitembelea kaburi la kamanda Soleimani akisema kuwa vikosi vya nchi yake vitalipiza kisasi kwa muda wake.
"Maadui zetu wataona nguvu ya Iran na ulimwengu mzima utafahamu juu ya uwezo na nguvu yetu. Vikosi vyetu vitaamua mahali na muda wa kuchukua hatua".
Karibu watu 100 waliuawa kwenye mashambulizi hayo yaliyotokea kwenye kumbukumbu ya miaka minne ya mauaji ya kamanda wa juu wa jeshi la mapinduzi Qassem Soleimani aliyeuawa nchini Iraq mwaka 2020 kwa ndege ya Marekani isiyo na rubani.
Soma pia: Iran yaapa kulipa kisasi kwa shambulio la bomu huko Kerman
Licha ya kundi linalojiita Dola la Kiislamu IS kudai kuhusika na mashambulizi hayo, maafisa wa Iran wameendelea kuzituhumu Israel na Marekani. Mkuu wa jeshi la wanamapinduzi la Iran Hossein Salami alisema kwenye mazishi hayo kuwa kundi la IS "limetoweka", na kuongezea kuwa kwa hivi sasa linatumika kama mamluki tu kwa maslahi ya Marekani na Israel.
"Ikiwa nyinyi mtaishi miaka elfu moja, tutawapata popote mlipo. Kwahiyo, nawaambia wairan leo kwamba tuko kwenye vita vikali lakini niwahakikishie tutawashinda. Muwe na uhakika kwamba hatutamruhusu adui atudhibiti hata kidogo."
Soma kuhusiana: Iran yaomboleza kifo cha kamanda wa walinzi wa mapinduzi
Marekani imekana yenyewe na mshirika wake mkuu Israel kuhusika na mashambalizi hayo. Wakati huo huo wizara ya mambo ya ndani ya Iran imetangaza baadae kuwa "baadhi ya watu wanaoshukiwa kuhusika kwenye shambulizi wamekamatwa".
Naibu waziri wa mambo ya ndani Majid Mirahmadi alisema kuwa "watu mbalimbali wamekamatwa katika miji mitano katika mikoa mitano, ambao wanashukiwa kuhusika na milipuko hiyo.