1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran na Venezulea zasaini ushirikiano wa miaka 20

11 Juni 2022

Venezuela na Iran zimesaini makubaliano ya ushirikiano kwa miaka 20 ikiwa ni siku moja baada ya rais Maduro kuisifu Jamhuri ya kiislamu ya Iran kwa kuipelekea nchi yake mafuta licha ya vikwazo vya Marekani.

https://p.dw.com/p/4CZVR
Iran | Venezuela | Besuch von Ebrahim Raisi bei Präsident Maduro
Picha: ENTEKHAB

Katika mahojiano na rais Maduro baada ya kuwasili kwake mjini Tehran kwa ziara ya siku mbili,kituo cha habari cha taifa cha Iran kiliripoti ijumaa usiku kwamba Maduro ameisifu hatua ya Iran ya kupeleka mafuta nchini Venezuela.  Maduro alisema hatua hiyo ya Iran ni msaada mkubwa kwa wananchi wa Venezuela.

Ziara hiyo ya kwanza ya rais Maduro nchini Iran imekuja wakati ikiwepo mivutano kote katika eneo la Mashariki ya kati kuhusu kuvunjika kwa mkataba wa Nyuklia wa Iran na mataifa yenye nguvu duniani. Vikwazo vya Marekani pamoja na ongezeko kubwa la bei ya vyakula duniani vinauumiza uchumi wa Iran ambao tokea hapo unayumba, na kuongeza shinikizo zaidi dhidi ya serikali yake na wananchi. Katika ziara yake rais Maduro anaandamana  na ujumbe wa ngazi ya juu wa kisiasa na kiuchumi kutoka Venezuela  ambayo kama ilivyo Iran inakabiliwa na vikwazo vya Marekani.Rais Maduro alialikwa na rais Ebrahim Raisi.

Ushrikiano wa Iran na Venezuela utajikita katika sekta ya mafuta na ulinzi.

Venezuela | Iranische Präsident Ebrahim Raisi besucht Nicolas Maduro
Marais Nicolas Maduro na Ebraihim RaisiPicha: Vahid Salemi/AP Photo/picture alliance

Katika mkutano wa pamoja na waandishi habari uliofanyika leo Jumamosi viongozi hao wawili Raisi na Maduro walisaini makubaliano ya miaka 20 ya ushirikiano utakaotanua uhusiano wao katika sekta ya mafuta na usafishaji mafuta ghafi,kijeshi na uchumi.

Aidha imeelezwa kwamba viongozi hao wawili watajadiliana kuhusu haja ya kuzifahamisha zaidi nchi zao kuhusu vita ya vikwazo na kutafuta njia  ya kukabiliana na vikwazo hivyo hivyo katika hali ya uthabiti.Maduro amesema Venezuela na Iran zimeungana zikiwa na dhamira ya pamoja katika masuala ya kimataifa na zote mbili ni wahanga hatua za kionevu zilizochukuliwa na Marekani na washirika wake.

Soma zaidi: Biden aunga mkono mazungumzo kati ya Maduro na upinzani

Rais huyo wa Venezuela amesema Caracas na Tehran zimejenga mkakati wa uchumi usiotikisika na wanashirikiana kutanua mkakati huo.Maduro yuko kwenye ziara katika eneo la kaskazini la  Ulaya na Asia baada ya rais Joe Biden kuamua kutomualika kwenye mkutano wa kilele wa nchi za Amerika ulioanza alhamisi wiki hii.Rais Maduro mwanzoni mwa wiki hii alikuweko pia Algeria na Uturuki.

Chanzo: AFP

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW