Iran: Marekani ioneshe nia kufufuliwa mkataba wa nyuklia
20 Septemba 2023Akihutubia Hadhara Kuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, kiongozi huyo wa Iran amesema uamuzi wa Marekani wa kujitoa kwenye mkataba huo ulikuwa ni ukiukaji wa makubaliano yenyewe na Washington inafaa kuonesha nia ya uhakika wakati inapigia debe kufufuliwa kwa utekelezaji wake.
Rais Joe Biden wa Marekani alijaribu kuanzisha mashauriano ya kuufufua mkataba huo muda mfupi baada ya kuingia madarakani lakini juhudi hizo zimesimama kwa karibu mwaka mmoja baada ya Iran kukataa mapendekezo ya wapatanishi wa Umoja wa Ulaya.
Wanadiplomasia wa mataifa ya magharibi wanaamini siyo rahisi tena kuufufua mkataba huo wa mwaka 2015, kwa sababu Iran imekiuka masharti mengi ikiwa ni pamoja na kuongeza urutubishaji wa madini ya Urani kwa ajili ya mradi wake wa nyuklia.