Iran kukiuka makubaliano ya nyuklia
7 Julai 2019Hali ya wasiwasi ikiwa inaongezeka, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amekosoa uamuzi huo wa Iran na kusema kwamba unakiuka makubaliano hayo ya nyuklia ambayo Marekani iliamua kujiondoa mwaka uliopita.
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema hatua hiyo ni ya hatari sana na amezitaka nchi za Ulaya kuiadhibu Iran kwa kuiwekea vikwazo.
Katika mkutano na wanahabari, maafisa wakuu wa serikali ya Iran wamesema kuwa Iran itaendelea kupunguza uzingatiaji wake wa mkataba huo baada ya kila siku 60 iwapo mataifa yaliotia saini mkataba huo hayatachukuwa hatua za kuilinda dhidi ya vikwazo vya Rais wa Marekani Donald Trump.
"Tumejitayarisha kikamilifu kurutubisha madini ya urani kwa kiasi chochote kile," amesema Behrouz Kamalvandi, msemaji wa Shirika la Nishati ya Atomiki Iran.
"Katika masaa machache yajayo ulimbikizaji wa madini ya urani wa kupindukia asilimia 3.67 utaanza kutekelezwa," akikusudia kikomo kilichoafikiwa katika makubaliano ya nyuklia ya 2015.
Iran hata hivyo imesema wakati wowote iko tayari kubadilisha uamuzi wake. Hatua zote zilizochukuliwa na Iran katika kupunguza ushirikiano wa mkataba wa nyuklia zinaweza kusitishwa mara moja iwapo mataifa ya Ulaya yaliyoweka saini makubaliano hayo yatatimiza majukumu yake, ameandika Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Javad Zarif, katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter.
Waziri Mkuu wa Israel ambaye ni mkosoaji mkubwa wa makubaliano hayo ya nyuklia ya 2015, amesema kurutubishwa kwa kiwango cha madini ya urani kuna lengo moja tu nalo ni kutengeneza mabomu ya atomiki.
Masharti ya makubalino
Mshauri mkuu wa Kiongozi wa Kidini wa Iran Ayatollah Ali Khamenei amesema Jumamosi kwamba kiongozi huyo anaunga mkono uamuzi wa serikali ya Iran.
Chini ya makubaliano hayo ya 2015, Iran ilikubali kulimbikiza madini ya urani kwa hadi asilimia 3.67, ambayo ni chini ya asilimia 20 iliyokuwa ikirutubishwa kabla ya makubaliano hayo na chini ya asilimia 90 inayohitajika kutengeneza silaha za nyuklia.
Kamalvandi amesema Iran itarutubisha urani kwa ajili ya vinu vyake vya umeme vya Bushehr, hadi kufikia 5%, tamko ambalo linathibitisha ripoti za Jumapili za shirika la habari la Reuters.
Iran haioneshi dalili yoyote ya kutishika kutokana na shinikizo la Marekani ambalo limechukua mtazamo wa kijeshi. Marekani inailaumu Iran kwa kuhusika na mashambulizi dhidi ya meli za kubebea mafuta pamoja na kudungua ndege yake isiyotumia rubani. Madai ambayo Iran inayakanusha. Madai hayo ya Marekani yalepelekea rais Trump kutishia kufanya mashambulizi ya anga dhidi ya Iran uamuzi alioubadilisha kabla ya kutekelezwa.
Mahusiano tete ya muda mrefu kati ya Marekani na Iran yalizidi kusambaratika mnamo Mei 2018 kufuatia Trump kuiondoa Marekani katika makubaliano ya kinyuklia ya 2015 pamoja na kuiwekea tena vikwazo.
Trump anadai kwamba makubaliano hayo ni dhaifu kwasababu baadhi ya masharti yake sio ya kudumu, na pia kwasababu makubaliano hayo hayagusi masuala yasiyohusu silaha za nyuklia kama vile mpango makombora ya masafa marefu pamoja na nia ya Iran kujiongezea ushawishi katika kanda ya Mashariki ya Kati.
Iran yazishinikiza nchi za Ulaya
Mvutano kati ya Iran na Marekani ni mtihani mkubwa kwa diplomasia ya nchi za Ulaya. Mataifa hayo ya Magharibi ambayo yalikosoa vikali uamuzi wa Trump mwaka uliopita wa kujitoa katika makubaliano hayo, yameiomba Iran kuendelea kuheshimu masharti ya makubaliano hayo.
Lakini Iran imeeleza kwamba haiwezi kuvumilia namna nchi za Ulaya zilivyoshindwa kuulinda uchumi na maslahi ya nchi yake dhidi ya vikwazo vya Marekani.
"Nchi za Ulaya zimeshindwa kutekeleza ahadi zao kwahiyo nao pia wanahusika, " amesema Abbas Araqchi, mjumbe mwandamizi wa Iran katika suala la makubaliano ya nyuklia, akizungumza na waandishi habari mjini Tehran.
Iran inasema mpango wake wa nyuklia una madhumuni ya amani, kama vile kuzalisha umeme, na sio kutengeneza mabomu ya nyuklia.
Chanzo (rtre,ap)