IOM: Idadi ya wakimbizi wa ndani Sudan yapindukia milioni 10
11 Juni 2024Matangazo
Msemaji wa IOM, Mohammedali Abunajela amesema zaidi ya watu milioni mbili wamelazimika kukimbilia mataifa kama Chad, Sudan Kusini na Misri, na wengine milioni 2.8 waliyakimbia makazi yao kabla ya hata ya vita hivi vya sasa. Vita hivyo vimeiharibu Sudan na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 14,000 na kujeruhi maelfu, huku ikiwaingiza raia katika hali ya njaa kali. Mwezi uliopita, Shirika la chakula la Umoja wa Mataifa lilionya pande zinazopigana kwamba kuna hatari kubwa ya kuenea kwa njaa na vifo katika eneo kubwa la magharibi mwa Darfur na kwingineko nchini Sudan ikiwa hawataruhusu misaada ya kibinadamu.