India yazidi kuandamwa na kiwingu cha COVID-19
6 Julai 2020Wizara ya Afya ya India imesema katika muda wa saa 24 zilizopita, imekuwa na maambukizi mapya 24,000 na hivyo kufanya jumla ya idadi ya walioambukizwa nchini humo hadi sasa kufikia 697,358, mnamo wakati Urusi ikiwa na visa 681,000
Marekani na Brazil ndizo zinaongoza kwa idadi ya juu ya maambukizi. Hata hivyo, haitarajiwi kuwa India itafikia kilele chake baada ya wiki kadhaa japo wataalamu wa afya wametabiri kuwa idadi ya maambukizi ya India itapindukia watu milioni moja mwezi huu.
Watu 19,963 wamefariki nchini India kutokana na COVID-19, hiyo ikiwa ni idadi ya chini ikilinganishwa na mataifa yaliyoathiriwa pakubwa.
Miji iliyoathiriwa zaidi nchini India na janga hilo ni New Delhi pamoja na Mumbai, kila mji ukiwa na zaidi ya maambukizi 100,000.
Sherehe za Uhuru zafutwa nchini Malawi
Huko Malawi rais mpya Lazarus Chakwera amefutilia mbali sherehe zilizopangwa za uhuru na vilevile amepunguza pakubwa sherehe za kuapishwa kwake, kutokana na kuongezeka kwa maambukizi ya virusi vya corona katika taifa hilo la kusini mwa Afrika.
Sherehe rasmi ya kuapishwa kwa Chakwera ilipaswa kufanywa leo katika uwanja mkubwa mjini Lilongwe, na ilipaswa kuenda sambamba na sherehe za kuadhimisha miaka 56 ya uhuru.
Malawi imerekodi visa 1,613 vya maambukizi ya corona na haijaweza vizuizi.
Katika hotuba yake siku ya Jumapili, Rais Chakwera alisema sherehe ya kuapishwa kwake sasa itafanyika katika kambi ya kijeshi na watu 100 pekee walioalikwa ndio watahudhuria.
Chakwera alishinda uchaguzi wa rais uliorudiwa Juni 23 kwa kupata asilimia 58.5 ya kura, dhidi ya aliyekuwa rais Peter Mutharika.
Hatua ya kupunguza sherehe hizo imepunguza furaha ya watu waliotaka kusherehekea ushindi huo wa kihistoria, baada ya mahakama kufutilia matokeo ya uchaguzi wa mwaka uliopita ambapo Peter Mutharika alitangazwa mshindi.
Misri inatumia vitisho dhidi ya wataalamu wa afya
Mamlaka nchini Misri imewakamata wahudumu wa afya baada ya wahudumu hao kuandika wakihoji jinsi janga la corona linavyoshughulikiwa nchini humo.
Watu hao waliokamatwa ni daktari mmoja ambaye aliandika nakala kuhusu udhaifu wa mfumo wa afya nchini Misri, mwengine ni mfamasia aliyechukuliwa kutoka kazini kwake baada ya kuchapisha mtandaoni juu ya uhaba wa mavazi ya kujikinga.
Wengine ni mhariri aliyehoji juu ya takwimu za maambukizi ya corona pamoja na daktari mjamzito aliyekamatwa baada ya mwenzake kutumia simu yake kuripoti juu ya mtu aliyeshukiwa kuambukizwa virusi vya corona.
Vyombo vya usalama nchini Misri vinajaribu kuzuia ukosoaji wa serikali ya Rais Abdel Fattah el-Sissi inavyolishughulikia janga hilo la kiafya.
Kulingana na makundi ya kutetea haki za binadamu nchini Misri, madaktari wapatao 10 na waandishi wa habari sita wamekamatwa tangu virusi vya corona viliporipuka nchini humo mnamo mwezi Februari.