India kwenye maonyesho ya vitabu ya Ujerumani
4 Oktoba 2006India inaonekana kuwa nchi inayokuwa haraka kiuchumi. Hata hivyo, kwa upande wa vitabu, wasomaji wa Ujerumani wanavutiwa hasa na fasihi ngeni.
Waandishi kadhaa wa Kihindi wana umaarufu mkubwa kuliko miaka 20 iliyopita, kama vile Salman Rushdie, Vokram Seth au Arundhati Roy. Hata hivyo, wote watatu hawawawakalishi waandishi wa kawaida wa Kihindi, kwani wote hawa wana andika wa Kiingereza badala ya kutumia moja kati ya lugha ishirini za kienyeji zinazotumika kwa kuandika fasihi huko India.
Mtaalamu wa mambo ya Kihindi wa chuo kikuu cha Munich, Bibi Ira Sharma, alichunguza ni fasihi gani huuzwa katika maduka ya vitabu nchini Ujerumani: “Ile inayoonekana kuwa fasihi ya Kihindi, hasa ni vitabu vilivyoandikwa kwa Kiingereza na halafu kutafsiriwa Kijerumani. Vitabu ambavyo kwanza viliandikwa kwa lugha ya kienyeji, havitapata umaarufu. Tena fasihi ya Kihindi inasemekana kuwa ni vitabu vinavyohusu India. Maana yake ni kwamba vitabu vingi havikuandikwa na waandishi wa Kihindi, lakini ni riwaya zilizoandikwa na waandishi wa Ulaya au Marekani, lakini hadithi zao zinatokea huko India.”
Hadithi za kutoka India zinawavutia wasomaji wengi wa Kijerumani kwa sababu ni hadhiti za kigeni zenye ajabu. Kwa sababu hiyo makampuni ya uchapishaji yanapenda kuweka picha za pahali pa utalii kama jengo la Taj Mahal katika ukarasa wa kwanza hata ikiwa kitabu hiki hakihusu kabisa Taj Mahal.
Tatizo kuu la kuuza fasihi iliyoandikwa katika lugha za kienyeji ni ukosefu wa wafasiri mabingwa. Wale wanaotafsiri vitabu kutoka lugha ya Kihindi au Kibengali kwa Kijerumani hasa ni wasomi wa vyuo vikuu.
Shida yao lakini ni kwamba hawafahamu soko la vitabu vya Ujerumani, anasema Bibi Sharma: “Wajerumani wanapenda sana kusoma riwaya. Riwaya zinauzwa vizuri zaidi hapa nchini. Nchini India lakini waandishi wanapenda sana kuandika hadithi fupi au mashairi. Sasa, wasomi wa vyuo vikuu sana wanakusanya hadithi au mashairi mazuri katika vitabu. Lakini vitabu hivi havitauzwa nchini Ujerumani.”
Hata hivyo, maonyesho ya vitabu ya Frankfurt yanawapa fursa waandishi wengi wa India kujitambulisha kwa wasomaji wa Ujerumani. Juu ya vitabu vyao kuuzwa, wengi wao watapanda jukwaa kuhudhuria kwenye mazungumzo au kusoma vitabu vyao hadharaní. Hivyo, wasomaji wa Ujerumani wataweza kubadilisha mawazo yao kuhusu India.