India kuondoa baadhi ya vikwazo Kashmir
16 Agosti 2019Operesheni ya usalama katika Bonde la Kashmir, nyumbani kwa karibu watu milioni saba, imesababisha ukosoaji mkubwa na leo, Mahakama ya Juu ya India imesikiliza kesi iliyowasilishwa na mhariri wa gazeti aliyetaka huduma za mawasiliano zirejeshwe ili wanahabari wafanye kazi.
Anuradha Bhasin, mhariri mkuu wa Kashmir Times, aliwaambia wanahabari nje ya mahakama kuwa hangeweza kuwasiliana na wafanyakazi wake kwa sababu ya laini zote za simu pamoja na intanet zimekatwa.
Wakili wa serikali Tushar Mehta aliiambia mahakama kuwa maafisa wa usalama wanaitathmini hali hiyo na wanapaga kuondoa vikwazo hivyo katika siku chache zijazo.
Wakati huo huo, mwanajeshi mwingine wa Pakistan ameuawa katika makabiliano na wanajeshi wa India katika jimbo la Kashmir leo Ijumaa. Kifo hicho kinafikisha idadi ya vifo katika jimbo hilo linalogombaniwa watu sita katika saa 24 zilizopita.
Taarifa ya jeshi la Pakistan imesema askari wa India walifyatua katika eneo linalofahamika kama Eneo la Udhibiti, ambalo ni la mpaka unaolitenganisha bonde la Himalaya katika sehemu zinazodhibitiwa na nchi hizo mbili.
Karibu wanajeshi watatu wa Pakistan na raia wawili waliuawa Kashmir jana Alhamisi katika makabiliano ya kwanza ya risasi kati ya walinzi wa mpakani tangu serikali ya New Delhi ilipoifuta hadhi maalum ya upande wa India wa jimbo la Kashmir.
Jeshi la Pakistan limedai kuwa liliwauwa wanajeshi watano wa India katika majibizano ya risasi, lakini ripoti za vyombo vya habari vikiwanukuu maafisa mjini New Delho zinakanusha kutokea kwa vifo vyovyote kwa upande wao. Jeshi la India halijatoa taarifa rasmi kuhusu ripoti za makabiliano hayo.
Uamuzi wa India wiki iliyopita kuifuta hadhi maalum ya kikatiba ya Kashmir na kuweka operesheni ya usalama katika jimbo hilo umezusha mivutano mipya kati ya mahasimu hao wawili wa Kusini mwa Asia, ambao awali walipigana vita mara mbili kuhusu Kashmir.
Makabiliano haya ya karibuni yanakuja wakati Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa likitarajiwa kufanya kikao cha faragha kuamua kama litaitisha mkutano wa dharura wa kuijadili hali hiyo ya Kashmir kufuatia ombi la Pakistan