India inashika nafasi ya tatu kwa maambukizi duniani
6 Julai 2020Kuna ishara ya mafanikio katika baadhi ya maeneo ya Ulaya, ambapo makumbusho ambayo yanahudhuriwa na idadi kubwa ya watu duniani ya Louvre ya mjini Paris yanafunguliwa leo hii. Na hii inafanyika wakati jumla ya maambukizi inakaribia watu milioni 11.5 na vifo zaidi ya 533,000 duniani kote. Serikali ya India kama zilivyo nyingine nyingi duniani kote, imeanza kuondoa vizuizi vya kukabiliana na virusi hatua kwa hatua kwa lengo la kunusuru uchumi wa taifa hilo uliathiriwa.
Maambukizi mapya zaidi ya 24,000
Lakini idadi ya maambukizi imeendelea kupanda, kukiwa na visa 24,000 vilivyoripotiwa katika kipindi cha masaa 24, na hivyo kufanya idadi jumla ya maambukizi kufikia karibu watu 700,000. Miji mkubwa ya India ikiwemo New Delhi na Mumbai, ndio iliyoathirika zaidi.
Na wakosoaji wanasema vipimo vinafanyika kwa kiwango kidogo sana na visa vingi vya COVID-19 vimeshindwa kutambulika.
Nchini Australia, ambako ripoti zilionesha mripuko wa virusi vya corona umeweza kudhibitiwa, kumeibuka kisa kipya katika mji wa Melbourne, na kuilazimisha serikali kuliweka katika kizuizi maalumu jimbo la Victoria kwa lengo la kuyanusuru majimbo mengine.
Marekani taaifa ambalo limeathirika vibaya zaidi dunani, lipo katika jitihada za kupunguza athari za maradhi hayo katika kipindi hiki ambacho idadi ya vifo imekaribia watu 130,000 na jumla ya maambukizi milioni 2.8. Hali inakuwa hivyo huku pia katika maeneo mengi ambayo yameathiriwa vibaya na maambukizi hayo ikiwa yanalegeza masharti ya kupunguza maambukizi.
Vitanda vyafurika wagonjwa wa COVID-19 nchini Marekani
Wakati Rais Donald Trump akionesha hali ya kupuuza hali ilivyo nchini humo vitanda vinanoekana kujaa wagonjwa katika baadhi ya hospitali za Texas, huku miito mipya ya kusalia nyumbani ikiongezeka. Baadhi ya mameya wa miji wanasema baadhi ya miji imefunguliwa mapema mno.
Iran nayo imetangaza vifo vipya 163, ikiwa ni kiwango kikubwa kabisa kutangazwa kwa siku tangu kuanza kwa mripuko huo, wakati Morocco ikibaini kuzuka kwa mripuko huo katika eneo la kiwanda cha uvuvi wa samaki, ambapo wakazi takribani watu 300,000 wamewekwa kizuizini. Katika mataifa ya Amerika ya Kusini mapambano bado yanaendelea ambapo Chile inapindukia vifo 10,000 hadi Jana Jumapili, huku Mexico vifo 30,000.
Soma zaidi:Afrika kufungua anga huku corona ikizidi kusambaa
Afrika ya Kusini watoa tiba walitawanywa katika jimbo la East Cope hapo jana baaada ya kuzuka kiwango kikibwa cha maambukizi katika eneo la jimbo hilo.