1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Imran Khan mshindi uchaguzi Pakistan

Isaac Gamba
27 Julai 2018

Tume ya uchaguzi ya Pakistan imekitangaza chama cha nyota wa zamani wa mchezo wa kriketi Imran Khan kuwa mshindi wa katika uchaguzi wa bunge uliofanyika juzi na hivyo kukisafishia njia serikali ya tatu ya kiraia.

https://p.dw.com/p/32Bc1
Pakistan Imran Khan, neuer Premierminister
Picha: picture-alliance/Anadolu Agency/M. Reza

 Baada ya siku mbili ya zoezi la kuhesabu kura kumalizika, chama cha Imran Khan cha Tehreek-e-Insef, TIP, kimeshinda viti 109 miongoni mwa viti 269 vya bunge  huku mshindani wake wa karibu wa chama cha Pakistan Musilim League, Shahbaz Sharif, akishinda viti 63.

Sharif anayeongoza chama cha waziri mkuu wa zamani wa nchi hiyo, Nawaz Sharif, mapema aliyakataa matokeo ya uchaguzi huo akilalamikia udanganyifu.

Wapiga kura  katika taifa hilo linalofuata mfumo wa Uingereza wa bunge, Jumatano wiki hii waliwachagua wabunge wa mabunge yote mawili pamoja na mabunge manne ya majimbo.

Fawad Chaudhry, msemaji wa chama cha Imran Khan, alisema juhudi za kuunda serikali ya muungano tayari zimeanza lakini huenda zoezi hilo likachukua siku kadhaa.

Hapo jana Alhamisi, Imran Khan aliye na umri wa miaka 65, alitoa hotuba yake ya kwanza kabla ya hata kutangazwa rasmi kuwa mshindi na kuahidi kuliongoza taifa hilo katika hali ambayo haijawahi kushuhudiwa hapo kabla na kuapa kuondoa rushwa, kuimarisha taasisi pamoja na kuboresha mahusiano ya kimataifa kwa kuzingatia misingi ya heshima na usawa.

Hata hivyo, bado kuna safari ndefu kabla ya Pakistan kuuunda serikali kamili ili Imran Khan aweze kutekeleza hayo aliyoyaahidi.

Upinzani walalamikia matokeo

Pakistan Islamabad Fans von Cricket-Star-Politiker Imran Khan feiern Wahlsieg
Wafuasi wa Imran Khan wakishangilia ushindiPicha: Reuters/F. Mahmood

Washindani wa Khan pamoja na makundi ya haki za binadamu yanadai Khan ameshinda uchaguzi huo kwa njia za udanganyifu mkubwa, ikiwa ni pamoja na kulihusisha jeshi pamoja na taasisi ya kijasusi ya jeshi hilo kupanga matokeo, ingawa Imran Khan mwenyewe anasema uchaguzi huo umefanyika katika mazingira ya uwazi katika taifa hilo lenye historia ya miaka 71 na ambalo utawala wake kwa njia moja ama nyingine umekuwa  ukidhibitiwa na jeshi:

Chama cha Pakistan People's Party kinachoongozwa na mtoto wa waziri mkuu wa zamani aliyeuawa, Benazir Bhutto, kimeshika nafasi ya tatu baada ya kushinda viti 39 vya bunge. Bado matokeo ya viti 20 yanasubiriwa hii leo, ingawa hayatabadilisha matokeo ya jumla katika bunge la taifa lenye jumla ya viti 342, na ambalo  wabunge 272 ndio wanaochaguliwa moja kwa moja na wapiga kura.

Wakati tume ya uchaguzi nchini Pakistan ikikanusha madai ya kuwepo udanganyifu kwenye uchaguzi huo, waangalizi wa kimataifa wakiwemo wanaowakilisha Umoja wa Ulaya  leo Ijumaa wanatarajiwa kutoa tathimini yao kuhusiana na uchaguzi huo ikiwa ni baada ya vyama vingine vilivyoshiriki uchaguzi  kikiwemo chama kinachoondoka madarakani cha Pakistan, Musilim League, kudai matokeo yamepangwa.

Mwandishi: Isaac Gamba/APE/AFPE

Mhariri: Mohammed Khelef