IMF yatahadharisha kuhusu ruzuku za mabadiliko ya tabianchi
20 Januari 2023Mkuu wa shirika la fedha duniani IMF ametahadharisha kwamba ruzuku inayotolewa na nchi za Magharibi kupambana na mabadiliko ya tabia nchi na kuyatia shime mataifa ya ulimwengu kugeukia vyanzo vya nishati isiyoharibu mazingira, inatishia kuumiza uchumi wa nchi zinazoendelea duniani. Kristalina Georgieva akizungumza kwenye jukwaa la uchumi duniani mjini Davos amesema wasiwasi wake mkubwa ni kwamba mpango huo huenda usizisaidie nchi zinazoinukia kiuchumi na ulimwengu wa nchi zinazoendelea. Marekani chini ya rais Joe Biden imepitisha sheria ya kupunguza mfumko wa bei ambayo inajumuisha ruzuku kubwa na kuondowa kodi kwa kiasi dola bilioni 370 kwajili ya kupunguza uzalishaji gesi inayoharibu mazingira.Mpango huo ndio mkubwa zaidi wa kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi kuwahi kufanywa na Marekani. Georgieva ameonya kwamba ruzuku zinaweza kusababisha teknojia na uzalishaji kutoka nchi zinazoinukia kuhamishiwa kwenye nchi tajiri.