1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

IMF: Nchi zaombwa ziepuke kuwekeana vizingiti vya biashara

11 Aprili 2018

Hisa kwenye masoko ya Ulaya zimeyumba baada ya Mkurugenzi wa Shirika la Fedha la Kimataifa, IMF, Christine Lagarde, kutoa tahadhari juu ya vita vya kibiashara.

https://p.dw.com/p/2vsbx
Republik Belarus IWF Schild
Picha: DW/A.Timarov

Masoko makubwa ya hisa ya barani Ulaya yametetereka baada ya Mkurgenzi huyo wa IMF Christine Lagarde kuingilia Kati katika mzozo wa kibiashara baina ya Marekani na China Bi Lagarde ametahadharisha kwamba vizingiti vya kibiashara vitahujumu ustawi wa uchumi wa Dunia.

Masoko ya hisa ya London, Frankfurt na Paris yalipanda na kushuka yakiwepo matumaini kwamba vita vya kibiashara baina ya Marekani na China vitaepushwa. Akihutubia kwenye kongamano nchini China Mkurugenzi huyo wa shirika la fedha la kimataifa Christine Lagarde amesema ustawi wa uchumi wa dunia unaimarika lakini wakati huo huo ametahadharisha juu ya vita vya kibiashara.

Mkurugenzi wa Shirika la Fedha la Kimataifa IMF: Christine Lagard
Mkurugenzi wa Shirika la Fedha la Kimataifa IMF: Christine LagardePicha: picture alliance/abaca/M. Wondimu Hailu

Mkurugenzi huyo wa Shirika la Fedha la Kimataifa ameeleza kuwa ni kosa kuzingatia nakisi za biashara kuwa ni ishara ya biashara isiyokuwa ya haki kama ambavyo rais Trump amekuwa anadai mara kwa mara kama jinsi inavyoshuhudiwa sasa katika mzozo na China.

Katika kile kinachoonekana kuwa onyo la kificho kwa rais wa Marekani Donald Trump, ambaye kwa sasa anavutana na China kuhusu masuala ya biashara, bibi Lagarde amesema nchi zinapaswa kuweka biashara zao wazi zaidi, kwa kufanya mageuzi ya ndani badala ya kuweka vizingiti. Lagarde amesema serikali zinapaswa kuendesha sera za kujiweka mbali na vita vya kibiashara. Ametahadharisha kwamba mfumo wa sheria na wa wajibu sasa umo katika hatari ya kusambaratika.

Rais wa China Xi Jinping
Rais wa China Xi JinpingPicha: picture-alliance/Xinhua/Li Xueren

Hata hivyo rais wa China Xi Jinping ameituliza dunia baada ya kutoa kauli ya maridhiano na kuahidi kuiweka wazi zaidi milango ya kiuchumi ya nchi yake. Jinping amesema China itapunguza ushuru unaotozwa kwa magari na pia itachukua hatua ili kulinda haki miliki. Kauli ya rais wa China Xi Jinping imepunguza wasiwasi juu ya kufumuka vita vya kibiashara vinayvoweza kuvuruga uchumi wa dunia wakati ambapo uchumi huo unarejea katika hali ya kawaida baada ya mgogoro mkubwa wa mabenki wa hivi karibuni.

Vilevile hatua zilizotangazwa na rais huyo wa China zinayazingatia malalamiko yaliyotolewa na rais Trump na pia zimechukuliwa baada ya Marekani kutangaza duru nyingine ya ushuru kwa biadhaa za China zenye thamani ya mabilioni ya dola.

Rais wa Marekani Donald Trump
Rais wa Marekani Donald TrumpPicha: picture alliance / Newscom

Katika hatua ya kutia moyo rais wa Marekani Donald Trump amemshukuru rais Jinping kwa kauli yake nzuri. Trump amesema katika mtandao wa Twitter kwamba China na Marekani zitapiga hatua kubwa kwa pamoja. Rais wa China ametoa kauli hiyo nzuri baada ya Marekani na nchi yake kutoleana vitisho vya kulipizana kisasi kwa kila mmoja kusema kwamba atazitoza ushuru bidhaa za upande mwingine.

Mwandishi: Zainab Aziz/AFPE/RTRE

Mhariri: Mohammed Khelef