IMF, Benki ya Dunia waanza mkutano mkuu
9 Oktoba 2012Viongozi wa dunia wanawasili Tokyo kwa mkutano huo wa kila mwaka wa taasisi kubwa za kifedha duniani, katika wakati huu ambapo unaonesha kushindwa vibaya kwa wanauchumi na wanasiasa wa dunia kuinusuru hali. Kwa mujibu wa mkuu wa IMF, Christine Lagarde, uchumi wa dunia upo kwenye hali mbaya sana.
“Uchumi wa dunia umezingirwa na hali ya kutokuwa na utulivu, uko mbali sana na pale ulipopaswa kuwa. Hali hii ni kama vile mchezo wa bao la kete, ambapo kete zinaangukia kwenye mashimo yake lakini bao zima hadi sasa halijajaa.” Amesema Lagarde.
Kama bao la kete ndivyo ilivyo hasa hali ya uchumi wa dunia kwa sasa. Kwa mujibu wa utabiri wa karibuni kabisa wa IMF uliochapishwa leo, ukuwaji wa uchumi utashuka chini katika mwaka 2013.
Hata mataifa yaliyoendelea yako hatarini kuingia kwenye mgogoro wa kiuchumi, hali ambayo inasambaa kwa mataifa yanayoinukia, kama vile China, India na Brazil.
IMF watoa utabiri mpya
Miezi mitatu iliyopita, IMF ilikisia kuwa uchumi wa dunia ungelikuwa kwa asilimia 3.9, lakini sasa inasema utaongezeka kwa asilimia 3.6 tu. Utabiri wa ukuwaji wa Ujerumani unabakia kuwa asilimia 0.9 na unatarajiwa kubakia hivyo kwa mwaka mzima.
Lagarde anayataja mashimo yasiyojaa kwenye bao la kete la uchumi wa dunia hivi sasa wakati mkutano wa IMF na Benki ya Dunia ukianza, kuwa ni pamoja na "kuongezeka kwa nakisi katika hazina za kanda ya euro, kushindwa kuinuka kwa uchumi wa Marekani, kuzorota katika masoko yanayoinukia, wasiwasi mkubwa kwa nchi zenye pato la chini kuhusiana na kupanda kwa bei za vyakula na bidhaa muhimu kwa maisha."
Suala la kuendelea kwa fadhaa kwenye Mashariki ya Kati pia, anasema Lagarde, ni mambo yanayoutia mashakani uchumi wa dunia.
Hata hivyo, Lagarde amepongeza hatua zinazochukuliwa na benki kuu duniani, hasa barani Ulaya, Marekani na Japan, katika kuusaidia uchumi unaozorota, ikiwemo sera za kuingilia kati kifedha. Benki hizo zinatajwa kufanya kazi kubwa ya kuinusuru dunia dhidi ya mtikisiko mkubwa wa kiuchumi.
Mageuzi kwenye IMF
IMF inataka kuutumia mkutano huu wa Tokyo kujipanga vyema kwa majukumu makubwa yaliyoko mbele yake, likiwemo la kuisaidia dunia kupambana na upungufu wa ajira, kuimarisha nyenzo zake za uchambuzi wa hali ya uchumi duniani, kuwa na mfumo wa kutoa tahadhari mapema na kuwa na mtandao salama zaidi wa masoko ya kifedha duniani.
Kkubwa kuliko yote, hata hivyo, ni mageuzi ya kimuundo na kisera ndani ya IMF yenyewe. Mkutano huu wa Tokyo una dhima ya kutekeleza kile ambacho mataifa ya G20 yaliamua miaka miwili iliyopita, nalo ni kugawanywa kwa haki ya kupiga kura kwa kuyapa nafasi masoko yanayoinukia na mataifa yanayoendelea, kwa asilimia sita zaidi na hivyo kufikia sasa asilimia 45. China itaongeza kasma yake mara mbili zaidi na kwa mara ya kwanza India na China zitakuwa kwenye orodha ya nafasi kumi za juu.
Mwandishi: Rolf Wenkel/Mohammed Khelef/DW
Mhariri: Oummilkheir Hamidou