Idriss Deby Itno ashinda uchaguzi Chad
10 Mei 2024Matokeo hayo yamepingwa na mpinzani wake mkuu Succes Masra. Matokeo hayo yaliyokuwa yanatarajiwa Mei 21, yametolewa wiki moja mapema, na yamemuonesha Deby Itno akiwa na asilimia 61 ya kura huku Masra akipata asilimia 18.5 ya kura hizo. Kumesikika milio ya risasi N'djamena baada ya matokeo hayo kutangazwa.
Chad ilifanya uchaguzi wake baada ya kucheleweshwa kwa muda mrefu, huku ikiwa chini ya utawala wa kijeshi kwa miaka mitatu. Wachambuzi wanasema walitarajia ushindi kwa Mahamat Deby Itno ambaye yuko madarakani.
Njama ya kuchakachua matokeo
Deby Itno alichukua madaraka baada ya babake aliyekuwa uongozini kwa kipindi cha miongo mitatu, kuuwawa katika mapambano na waasi mwaka 2021.
Nchi hiyo yenye utajiri wa mafuta na yenye idadi ya watu milioni 18, haijafanya uchaguzi huru na haki tangu ilipopata uhuru wake 1960 kutoka kwa Ufaransa.
Saa chache kabla kutolewa kwa tangazo hilo la tume inayosimamia uchaguzi wa Chad, Masra alichapisha hotuba katika mtandao wa kijamii wa Facebook, akizituhumu mamlaka nchini humo kwa njama ya kutaka kuchakachua matokeo.
Katika hotuba hiyo ya dakika 11, Masra alionekana amevalia koti la samawati akiwa amesimama kwenye jukwaa lililokuwa na bendera ya nchi hiyo nyuma yake, akidai kwamba yeye ndiye aliyeshinda uchaguzi.
Ametoa wito kwa jeshi la Chad, polisi na vikosi vingine vya usalama kutofuata maagizo ya Deby Itno. Hakukuwa na jawabu kuhusiana na madai hayo ya Masra kutoka ofisi ya rais wa nchi hiyo.
Rafiki wa mwisho wa Marekani na Ufaransa eneo la Sahel
Masra ambaye ndiye kiongozi wa chama cha The Transformers Party, aliikimbia Chad mnamo Oktoba 2022.
Wakati huo, serikali ya kijeshi ya Chad, ilikifungia chama chake na vyama vyengine 6 kutokana na maandamano ya kupinga uamuzi wa Deby wa kuongeza muda wake madarakani kwa miaka miwili zaidi. Zaidi ya watu 60 waliuwawa katika maandamano hayo.
Chad inaonekana na Marekani na Ufaransa kama rafiki wao wa mwisho mwenye uthabiti katika eneo zima la Sahel, kufuatia mapinduzi ya kijeshi katika nchi za Burkina Faso, Niger na Mali katika miaka ya hivi karibuni.
Tawala za kijeshi katika mataifa yote hayo zimewatimua wanajeshi wa Ufaransa na kuvigeukia vikosi vya mamluki wa Urusi kwa usaidizi wa kiusalama.
Vyanzo: DPA/AP