Idadi ya vifo vya tetemeko la Uturuki, Syria yafikia 5,000
7 Februari 2023Nchi mbalimbali kote ulimwenguni zimepeleka vikosi vya kusaidia katika juhudi za uokozi, nalo shirika la Uturuki la kushughulikia majanga limesema Zaidi ya wahudumu 24,400 wako katika maeneo yaliyoathirika. Lakini kutokana na ukubwa wa eneo lililopigwa na tetemeko hilo la Jumatatu na karibu majumba 6,000 kuthibitishwa kuporomoka nchini Uturuki pekee, juhudi zao ni ndogo mno.
Soma pia: Waliouawa katika tetemeko Uturuki na Syria wapindukia 4,000
Uturuki ina wanajeshi katika mkoa wake na Syria na imelipa jukumu jeshi kuongiza juhudi za uokozi, ikiwemo kujenga mahema kwa wasiokuwa na makazi na hospitali ya muda katika mkoa wa Hatay.
Meli ya jeshi la wanamaji imetia nanga katika bandari ya Iskenderun, ambako hospitali iliporomoka, ili kuwasafirisha walionusurika hadi mji uliokaribu wa Mersin.
Katika mji wa Kituruki wa Gaziantep, watu walipata hifadhi katika maduka, viwanja vya michezo, misikitini na vituo vya jamii. Kwa mujibu wa Orhan Tatar, afisa wa Shirika la Kitaifa la Kusimamia Majanga nchini Uturuki, kiasi ya watu 3,419 walikufa katika mikoa 10 ya Uturuki, huku Zaidi ya 20,000 wakijeruhiwa.
Eneo lililoathirika na tetemeko hilo lina ukubwa wa karibu kilomita 110,000 za mraba. Nchi yetu inaendelea kufanya shughuli za utafutaji na uokozi kwa kutumia kila mbinu. Kuna karibu jumla ya matetemeko madogo 285 yaliyofuata mpaka sasa, lakini yanaongezeka. Katika upande wa Syria, wizara ya Afya ya Syria imesema idadi ya vifo katika maeneo yanayodhibitiwa na serikali imefikia watu 1,602, huku wengine 1,450 wakijeruhiwa.
Katika upande wa kaskazini magharibi unaodhibitiwa na waasi, makundi yanayoendesha shughuli zao kule yamesema karibu watu 450 walikufa na wengine wengi wakajeruhiwa. Kanali Golan Vach ni kamanda anayeongoza kikosi cha uokozi kutoka Israel
Lengo letu ni kuokoa maisha. Tunaamini kuwa maisha bado yanaweza kuokolewa katika wakati huu. Mazingira ni magumu. Hali ya hewa ni baridi na uharibifu ni mkubwa sana.
Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki ametangaza siku saba za maombolezo ya kitaifa. Katika ahadi za karibuni kabisa za msaada wa kimataifa, Rais wa Korea Kusini Yoon Suk Yeol amesema anajiandaa kupeleka maramoja kikosi cha utafutaji na uokoaji cha watu 60 pamoja na bidhaa za matibabu na wanajeshi 50. Serikali ya Pakistan imesema inatuma ndege iliyobeba vifaa vya msaada na kikosi cha uokozi chenye watu 50. India imesema itapeleka vikosi viwili vya uokozi wakiwemo mbwa wa kunusa na maafisa wa matibabu.
Rais Joe Biden wa Marekani alipigia simu Erdogan kumpa salamu za rambirambi na msaada mwingine kwa mshirika huyo wa NATO. Ikulu ya White House imesema inatuma makundi ya utafutaji na uokozi kusaidia juhudi za Uturuki.
Mwandishi: Bruce Amani
ap, afp, dpa, reuters