1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Idadi ya vifo Pakistan kufuatia mafuriko yapindukia 200

19 Agosti 2024

Mamlaka za Pakistan zimesema zaidi ya watu 200 wamekufa nchini humo kufuatia mafuriko makubwa tangu kuanza kwa mvua kubwa za msimu wa mwezi Julai.

https://p.dw.com/p/4jdz1
Mafuriko Pakistan
Mtaalamu Mkuu wa masuala ya utabiri wa hali ya hewa Sardar Sarfraz amesema mvua kubwa zinatarajiwa kuendelea kote nchini humo hadi Agosti 25Picha: ARIF ALI/AFP via Getty Images

Shirika la kitaifa la kudhibiti majanga nchini Pakistan limesema karibu nusu ya watu 215 waliokufa ni watoto, huku wengine zaidi ya 400 wakiwa wamejeruhiwa.

Hadi sasa vikosi vya uokoaji vinataabika kuyaondoa maji katika miji iliyokumbwa na mafuriko na wamekuwa wakitumia mashua kuwasafirisha watu kutoka miji ya kusini ya Sukkur na Larkana ambayo imeathirika pakubwa.

Mtaalamu Mkuu wa masuala ya utabiri wa hali ya hewa Sardar Sarfraz amesema mvua kubwa zinatarajiwa kuendelea kote nchini humo hadi Agosti 25.

Mwaka 2022, mafuriko na magonjwa yatokanayo na janga hilo yaliua zaidi ya watu 2,000 nchini Pakistan.