1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Idadi ya mauwaji ya IS yatimia 3,000

Admin.WagnerD29 Juni 2015

Shirika la kutetea haki za binaadamu la Syria limesema kundi la kigaidi linalojiita Dola la Kiislamu IS, limesababisha takriban vifo 3,000 katika kipindi cha mwaka mmoja nchini Syria.

https://p.dw.com/p/1FosS
Islamischer Staat Hinrichtung in Syrien
Picha: picture-alliance/ Balkis Press/ABACAPRESS.COM

Kwa mujibu wa shirika la kuetea haki za binadamu la Syria kundi la kigaidi linalojiita Dola la Kiislamu IS, limefanya mauwaji ya takriban watu 3,000 nchini Syria. Pamoja na kujeruhi mamia ya raia, tangu Juni ya mwaka jana.

Shirika hilo lilioko nchini Uingereza ambalo linafuatilia mgogoro wa Syria kupitia wanaharakati walioko nchini humo, limethibitisha kuwa kundi la IS limefanya mauwaji 3,027 kati yao ni raia 1,787 na watoto 74. Idadi hii ni katika kipindi cha mwaka mmoja, tangu Juni ya 2014.

Nusu ya watu waliuliwa na kundi hilo ni wa madhehebu ya Sunni wa kabila la Shaitat, ambao ni wapinzani wa kundi hilo.

Idadi hiyo pia inajumuisha mauwaji yaliyofanywa na kundi hilo la IS wiki hii, katika mji wa Kobani. Shirika hilo limeripoti katika kipindi cha wiki moja tu, IS iliuwa takriban watu 223 mjini humo.

Shirika hilo limesema pia kundi la IS limeuwa wanamgambo kadhaa ambao ni wapinzani wao wa makundi mengine ya uasi, wapiganaji kadhaa wa Kikurdi, pamoja na wanajeshi karibu 900 wa vikosi vya serikali.

Mashambulizi ya IS katika nchi tatu

Halikadhalika Ijumaa iliyopita kundi hilo la kigaidi pia lilifanya mashambulizi matatu katika nchi tofauti, na kutangaza rasmi kuhusika na mashambulizi hayo.

Mashambulizi hayo ni pamoja na lile lililotokea mjini Sousse, Tunisia. Mshambuliaji aliyejihami kwa bunduki alifyatua risasi na kuuwa watu 39, ikiwamo watalii wa nchi tofauti pamoja na raia katika hotel maarufu ya kitalii nchini humo.

Kuwait Anschlag Beerdigung
Mazishi ya waliofariki katika shambulizi la KuwaitPicha: picture-alliance/dpa/R. Qutena

Siku hiyo hiyo pia kundi la kigaidi la IS lilihusika na shambulizi lililotokea nchini Kuwait, katika msikiti wa Kishia wakati wa sala ya Ijumaa. Mshambuliaji wa kujitoa muhanga aliyejiripuwa kwa mabomu, alisababisha vifo vya watu 27 katika msikiti huwo.

Na shambulizi la tatu lililofanywa na kundi hilo siku hiyo hiyo ya Ijumaa iliyopita ilikuwa ni mjini Paris, Ufaransa. Shambulizi hilo lilifanywa na mtuhumiwa anayejulikana kwa jina la Yassin Salhi, aliyamuua kwa kumkata kichwa muajiri wake kwenye kiwanda kimoja cha kutengeneza vifaa vya anga mji wa Lyon. Kiwanda hicho kinamilikiwa na Marekani.

Kwa mujibu wa ripoti ya hivi karibuni ya Umoja wa Mataifa, zaidi ya watu 60,000 wamelazimika kukimbia makaazi yao nchini Syria. Wanamgambo hao wa jihadi wenye misimamo mikali ya dini ya Kiislamu, kwa sasa wanadhibiti maeneo makubwa katika nchi za Syria na Iraq.

Mwandishi: Yusra Buwayhid/dw

Mhariri:Iddi Ssessanga