1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ICJ yatambua hatari ya kimbari Ukanda wa Gaza

26 Januari 2024

Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) imetambua hatari ya kuwepo mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Gaza, japo katika uamuzi wake leo haikuiamuru Israel kusitisha oparesheni zake za kijeshi kwenye Ukanda huo.

https://p.dw.com/p/4bj9s
ICJ hukumu ya Israel
Jopo la majaji wa Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) wakati wa kusomwa uamuzi wa mahakama hiyo kwa kesi ya Afrika Kusini dhidi ya Israel.Picha: Piroschka van de Wouw/REUTERS

Katika uamuzi wa awali kwa kesi iliyowasilishwa na Afrika Kusini, Mahakama hiyo ya juu zaidi ya Umoja wa Mataifa imeiagiza Israel kuchukua hatua zaidi za kuwalinda Wapalestina ili kuzuia mauaji ya kimbari.

"Kwa kuzingatia hitimisho hili, mahakama haiwezi kukubaliana na ombi la Israel la kutaka kesi dhidi yake iondolewe." Alisema Rais wa ICJ, Jaji Joan E. Donoghue, wakati akisoma hukumu hiyo.

Soma zaidi: Israel: Kesi ya mauaji ya Kimbari haina hoja za msingi

Hata hivyo, majaji hao wameidhinisha sehemu tu ya matakwa ya Afrika Kusini ambayo ilikuwa inahimiza kusitishwa mara moja kwa oparesheni za kijeshi za Israel katika Ukanda wa Gaza.

Mahakama hiyo ya mjini The Hague, Uholanzi, imeamua kuwa Israel inapaswa kuchukua hatua za kuwalinda raia na kuruhusu misaada ya kibinaadamu.

Lakini Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, amekosoa uamuzi huo, na kusisitiza kuwa mashtaka ya Afrika Kusini siyo tu ya uongo, bali pia ni ya kukasirisha yanayostahiki kukataliwa "na watu wote wenye heshima duniani."