IAEA yatatua masuala ya nyuklia na Iran
30 Mei 2023Likinukuu vyanzo vyenye ufahamu juu ya suala hilo, shirika la habari la IRNA limesema IAEA imefunga uchunguzi wake kuhusu ugunduzi wa hivi karibuni wa chembechembe za urani zilizorutubishwa hadi asilimia 87.3.
Ripoti ya IAEA ya robo mwaka mnamo mwezi Machi, ilikuwa imesema kuwa wakaguzi waligundua chembechembe za madini hayo katika kinu cha nyuklia cha Fordo kilichoko chini ya ardhi na kuibua wasiwasi kutokana na urutubishaji wa hadi asilimia 90 wa madini yanayoweza kutengeneza silaha.
Ripoti hiyo imetolewa siku chache tu kabla ya mkutano uliopangwa wa bodi ya magavana wa IAEA, ili kutathmini upya ufanisi katika kushughulikia maswala yaliyosalia ya shirika hilo.
IAEA ilikuwa imeripoti kupatikana kwa Urani hiyo katika maeneo matatu ambayo hayakutangazwa na Iran kama yaliokuwa na shughuli za nyuklia katika siku zilizopita hii ikiwa pigo kwa juhudi za kudumisha mkataba wa kihistoria wa mwaka 2015 kati ya Iran na mataifa yenye nguvu duniani.
Wakati huo huo, IRNA imeripoti kuwa IAEA pia imefunga uchunguzi kuhusu kupatikana kwa Urani katika eneo la Marivan, karibu na mji wa Abadeh, umbali wa kilomita 525 Kusini Mashariki mwa Tehran. Mara kwa mara, wachambuzi wamehusisha eneo hilo na mpango wa kijeshi wa siri wa nyuklia na kuishtumu Iran kwa kufanya majaribio makubwa ya nyuklia mwanzoni mwa miaka ya 2000.
Eneo la Marivan katika mkoa wa Kusini wa Fars, ni la kwanza kati ya maeneo matatu kushughulikiwa chini ya mpango wa utekelezaji uliokubaliwa kati ya Iran na IAEA mnamo mwezi Machi mwaka jana.
Maeneo mengine mawili ni Varamin na Turquzabad.
Wasiwasi wa IAEA kuhusu maeneo hayo ni moja kati ya vikwazo vilivyobakia vya kufufua mkataba huo wa nyuklia wa mwaka 2015 ambao ulibaki mashakani baada ya kujiondoa kwa Marekani mwaka 2018.
Shirika la Fars pia limeripoti kuwa Iran ilikuwa imeshughulikia masuala ya wasiwasi ya IAEA kuhusu kugunduliwa kwa Urani iliyorutubishwa kufikia kiwango cha kuunda silaha za nyuklia.
Soma pia: Mkuu wa IAEA aridhishwa mazungumzo na Iran
Iran imesema kurutubishwa kwa sampuli hiyo kufikia kiwango cha asilimia 83.7 huenda kulitokana na mabadiliko ambayo hayakutarajiwa katika mchakato huo wa urutubishaji kwasababu haikudhamiria kurutubisha Urani kwa zaidi ya asilimia 60, ambayo bado iko chini ya asilimia 90 inayohitajika kwa silaha za nyuklia.
Siku zote Iran imekanusha nia yoyote ya kutengeneza silaha za nyuklia na kusisitiza kuwa shughuli zake ni kwa matumizi ya amani.