Hungary yalegezewa masharti iunge mkono vikwazo kwa Urusi
31 Mei 2022Makubaliano hayo hayajumuishi katika vikwazo hivyo usafirishaji kwa njia ya bomba ambao Hungary inautegemea kupata mafuta yake kutoka Urusi. Makubaliano hayo yanalenga kupunguza mapato ya Urusi kufadhili vita ilivyovianzisha zaidi ya miezi mitatu sasa nchini Ukraine na kuwekewa vikwazo vikali zaidi vya Umoja wa Ulaya.
Waziri Mkuu wa Latvia Krisjanis Karins, amesema kuwa habari muhimu ni kwamba Umoja wa Ulaya bado umeungana katika azma yake ya kusimamisha vita vya uchokozi vya Urusi nchini Ukraine.
Msemaji wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya amesema kuwa marufuku ya uagizaji wa mafuta ya Urusi kwa njia ya bahari itatekelezwa kwa awamu katika kipindi cha miezi sita kwa mafuta ghafi na miezi minane kwa mafuta yaliosafishwa.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu wa Poland Mateusz Morawiecki amesema angependa kumuona rais wa Urusi Vladimir Putin ameondolewa kabisa kutoka ikulu ya Urusi. Wakati wa kongamano hilo la Umoja wa Ulaya mjini Brussels kuhusu vita nchini Ukraine, Morawiecki amekiambia kituo cha habari cha Sky News kwamba ikiwa bara Ulaya na ulimwengu huru utashindwa katika vita hivi, na kupoteza vita hivyo, hakutakuwa salama tena kwa sababu watakuwa chini ya vitisho na ulaghai kutoka kwa Putin. Morawiecki ameongeza kuwa Putin anawakilisha nguvu ya kikatili.
Huku hayo yakijiri, mwenyekiti wa Umoja wa Afrika ambaye pia ni rais wa Senegal Macky Sall, amewaambia viongozi wa Umoja wa Ulaya kwamba vizuizi vya Urusi dhidi ya bandari za Urusi vinafungua njia kwa majanga makubwa ya kuenea kwa uhaba mkubwa wa bidhaa na kupanda kwa bei zake kote barani Afrika . Katika hotuba yake kwa viongozi waliokusanyika mjini Brussels Jumanne (31.05.2022) kwa kongamano hilo linalolenga kuisaidia Ukraine, Sall amesema kusimamishwa kwa usafirishaji nje wa nafaka na mbolea kupitia bahari nyeusi kunaibua hali ya wasiwasi kwa taifa lililo na watu milioni 282 wasiokuwa na lishe bora. Sall amesema kuwa bei ya mbolea barani Afrika tayari imeongezeka mara tatu ikilinganishwa na 2021.
Sall ameongeza kuwa kulingana na baadhi ya makadirio, mavuno ya nafaka barani Afrika yatapungua kwa asilimia 20 hadi 50 mwaka huu na kwamba wangependa kuona hatua zimechukuliwa kuhakikisha usafirishaji wa nafaka na upatikanaji wa soko.