Hungary na Slovakia zapinga msaada wa kifedha Ukraine
27 Oktoba 2023Viongozi hao wawili wa Hungary na Slovakia walitoa matamshi yao katika mkutano wa kilele wa viongozi wakuu wa Umoja wa Ulaya, unaojadili bajeti ya Umoja huo kwa miaka minne ijayo. Migongano ilitokea ndani ya mkutano huo unaofanyika mjini Brussels kuhusu wapi pakuwekeza fedha katika bajeti yao ya pamoja.
Mkutano huo ulipendekeza kwamba wanachama wachangie zaidi katika bajeti hiyo, ili waweze kuipa Ukraine euro bilioni 50 na euro bilioni 15 nyengine kwaajili ya masuala ya uhamiaji. Na pendekezo jengine ni la kutoa euro bilioni 20 kwaajili ya msaada wa kijeshi kwa Ukraine.
Ulaya yataka eneo salama la kibinaadamu kuundwa Gaza
Masuala ya Bajeti kwa kawaida yanahitaji umoja lakini migawanyiko ilishuhudiwa katika mkutano huo. Waziri Mkuu wa Hungary Viktor Orban, alisema haungi mkono msaada zaidi kwa Ukraine mpaka pale atakapoona pendekezo linaloridhisha.
Awali Orban alikosolewa na baadhi ya viongozi wenzake wa mataifa 27 yanayounda Umoja wa Ulaya, kwa kukutana na rais wa Urusi Vladimir Putin nchini China mwezi huu, wakati Moscow ikiendelea na vita vyake nchini Ukraine huku Ulaya ikijaribu kuitenga.
Umoja huo unatarajiwa kufikia maamuzi mwezi Desemba, kuangalia tena bajeti yake ya mwaka 2021-27 ya thamani ya trilioni 1.1, ambayo tayari imeathirika kutokana na utumiaji wa dharura, uliofanyika wakati wa janga la COVID 19 na tangu pia Urusi, ilipoanzisha uvamizi wake wakijeshi Ukraine mwaka 2022.
Slovakia yasema msaada itakaotoa kwa Ukraine ni wa kibinaamau tu
Kwa upande mwengine Waziri Mkuu mpya wa Slovakia Robert Fico amesema haungi mkono tena Ukraine kupewa msaada ya kijeshi, akiongeza kuwa kile watakachochangia ni msaada tu wa kibinaadamu. Fico ameonya kuhusu ufisadi na dhidi ya kuendelea kutoa msaada wa kifedha kwa taifa hilo linalokumbwa na vita.
Mataifa mengine ya Ulaya Mashariki yalikataa kukubaliana na Rais wa Lithuania Gitanas Nauseda aliyesema kuwa euro bilioni 50 zilizopendekezwa kwa Ukraine hazitoshi.
Urusi imeivamia Ukraine kwa miaka miwili na zaidi na imeendeleza mashambulizi nchini humo.
Waziri Mkuu wa Estonia Kaja Kallas amesema kando na kuiunga mkono Ukraine bajeti ya Umoja huo, inapaswa kuangazia namna ya kuimarisha uwezo wa ulinzi wa Umoja wa Ulaya. Waziri Mkuu wa Ubelgiji Alexander De Croo, pia ameunga mkono kuwa pendekezo walilopewa kuhusu Ukraine halikubaliki.
Kingine ni kwamba upande wa kusini, Waziri Mkuu wa Ugiriki Kyriakos Mitsotakis, amesema nchi yake inahitaji fedha zaidi kushughulikia suala la uhamiaji. Ameyasema hayo wakati umoja huo ukiwa mbioni kukaza kamba katika mipaka yake ya nje ili kupunguza ujio wa wakimbizi kutoka Mashariki ya Kati na Afrika.
Chanzo: reuters/dpa