1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Huduma ya intaneti yaendelea kufungiwa DRC

Sylvia Mwehozi
2 Januari 2019

Huduma ya intaneti imeendelea kukatwa kwa siku ya tatu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambako serikali inadai imechukua hatua hiyo ili kuepusha machafuko baada ya baadhi ya wagombea kuanza kujitangazia kuongoza.

https://p.dw.com/p/3At19
Kongo Präsidentschaftswahl | Wahllokal in Kinshasa
Picha: Imago/Zuma Press

Upinzani umeishutumu serikali kwa kukata huduma za intaneti siku ya Jumatatu ili kuepusha harakati za kujitangazia matokeo ya mapema. Wagombea wakuu watatu wanaopewa nafasi akiwemo wa upande wa Rais Joseph Kabila na wawili wa upinzani, wote walidai kuongoza katika matokeo ya awali, baada ya kumalizika zoezi la upigaji kura siku ya Jumapili.

Mshauri wa masuala ya kidiplomasia wa Rais Kabila, Barnabe Kikaye Bin Karubi ameliambia shirika la habari la AFP kuwa Baraza la usalama la taifa limeamua kwamba ilikuwa "muhimu" kukatiza huduma za intaneti ili kuiruhusu tume ya uchaguzi kumaliza kuhesabu kura na kukamilisha matokeo.

"Kuna watu wamedanganya umma na taarifa za uongo kuhusu uchaguzi huu. Hili limeweka msingi wa kuanza kwa machafuko", alisema Karubi siku ya Jumanne. Karubi hakusema hadi lini huduma ya intaneti itakatizwa katika taifa hilo.

Kukatwa kwa huduma ya intaneti kumeleta athari kadhaa, ambapo wakazi wa mji wa Kinshasa walikuwa wakijaribu bahati zao kuipata huduma hiyo hasa katika mahoteli makubwa ambako huduma hiyo inaweza bado kuwa inapatikana. Baadhi yao walilazimika kununua vifurushi vya nchi jirani ya Jamhuri ya Congo.

Wahlen im Kongo
Rais Joseph Kabila mara baada ya kupiga kura siku ya Jumapili Picha: picture-alliance/AP/J. Delay

Idhaa ya radio ya Kifaransa nayo imeathiriwa na kadhia hiyo, ambapo serikali ilimnyang'anya kitambulisho ripoti wa idhaa hiyo Jumatatu jioni kwa madai ya kurusha matokeo yasiyo rasmi kutoka upinzani.

Nchi za magharibi zimeitaka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kurejesha huduma za intaneti. Pia wameunga mkono ombi la mashirika makubwa yanayofuatilia uchaguzi wa Congo kuweza kupata ruhusa ya kuingia katika vituo vya uchaguzi ambako kura zinahesabiwa tangu Jumapili.

Kauli hiyo ya pamoja ilitolewa na wakuu wa ujumbe wa Umoja wa Ulaya, Marekani, Canada na Uswisi mjini Kinshasa. "Tunaiomba serikali kuacha kuzuia njia za mawasiliano, hususan upatikanaji wa intaneti na vyombo vya habari", ilisema kauli yao. Kauli hiyo pia imeungwa mkono na nchi nyingine wanachama ikiwemo Ubelgiji, Uingereza, Ufaransa, Uholanzi na Sweden.

Mamlaka pia zimekata huduma ya ujumbe mfupi wa maandishi kwa njia ya simu, kwa mujibu wa kampuni ya Vodacom. Tume ya uchaguzi, CENI, ilisema matokeo rasmi yanatarajiwa kutangazwa siku ya Jumapili na rais mpya ataapishwa Januari 18. Wagombea watatu wa urais wanapewa nafasi ya kushinda, ambao ni Emmanuel Ramazani Shadari kutoka chama cha Kabila, Felix Tshisekedi kutoka UDPS na Martin Fayulu naye kutoka upinzani. Wote hawa tayari wamedai kuongoza katika uchaguzi wa Jumapili.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/AFP/reuters

Mhariri: Mohammed Khelef