HRW yaituhumu Misri kulazimisha kutoweka kwa mwanaharakati
3 Oktoba 2018Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu, Human Rights Watch limeitaka serikali ya Misri kufafanua alipo mwanasheria mtetezi wa haki za binadamu ambaye hajaonekana tangu alipokamatwa.
Tarehe 4 mwezi uliopita wa Septemba, mahakama moja nchini Misri iliamuru kuachiwa huru mwanasheria huyo Ezzat Ghoneim na mwenzake Azzoz Mahgoub wakati uchunguzi dhidi yake ukiendelea, lakini hakuna kilichotokea na wote wawili bado hawajaonekana wala kusikika, tangu Septemba 13.
Human Rights Watch imesema leo hii kuwa polisi ya Misri imelazimisha kutoweka kwa Ghoneim, ambaye alikamatwa mwezi Machi akituhumiwa kupanga njama dhidi ya serikali.
Shirika hilo limemnukuu mke wa Ghoneim, Rasha, ambaye amesema mara ya mwisho alimuona mme wake akizuiliwa katika kituo cha polisi cha al-Haram Kusini mwa mji mkuu Cairo, tarehe 13 Septemba.
Wizara ya mambo ya ndani ya Misri imekataa kutoa taarifa yoyote kuhusu rai hiyo ya Human Rights Watch.