HRW yaitaka Ethiopia kurejesha huduma ya intaneti Oromia
9 Machi 2020Tangu Januari 3, serikali ya Ethiopia imekatiza huduma za mitandao ya simu za mkononi na simu za kawaida pamoja na huduma za intaneti katika maeneo ya Kellem Wellega Magharibi mwa Oromia, Wellega Magharibi na Horo Gudru Wellega.Katika eneo la Wellega Mashariki, wakazi waliripoti kuwa huduma za intaneti na mitandao ya kijamii zilikatizwa huku zile za kutuma ujumbe na kupiga simu zikipatikana katika miji mikubwa pekee.
Hatua ya kukatizwa kwa huduma hizo imetekelezwa katika maeneo yalioko chini ya udhibiti wa jeshi la serikali hiyo na inakuja wakati kukiwa na ripoti za operesehni za jeshi la serikali hiyo dhidi ya kundi lililojihami ambalo wakati mmoja lilipigwa marufuku la Oromo Liberation Front (OLF). Vyombo vya habari vimeripoti kwa uhakika kuhusu ukiukwaji wa haki za binadamu ikiwa ni pamoja na visa vya mauaji na vikosi vya serikali kuwashikilia watu wengi.
Kwa mujibu wa mkurugenzi wa shirika la Human Right Watch katika eneo la upembe mwa Afrika Laetitia Bader, hatua ya serikali ya Ethiopia ya kukatiza mawasiliano kwa ujumla katika eneo la Oromia inasababisha madhara kwa raia wa eneo hilo na inapswa kufutiliwa mbali mara moja. Laetitia ameendelea kusema kuwa vikwazo hivyo vinaathiri vibaya huduma muhimu , habari kuhusu matukio muhimu na uchunguzi wa hali za binadamu na huenda ikachangia hali ya kibinadamu kuwa mbaya zaidi.
Shirika hilo la Human Rights limesema kuwa chini ya uongozi wa waziri mkuu Abiy Ahmed, kukatizwa kwa mawasiliano bila sababu kumekuwa jambo la kawaida wakati wa ghasia za kijamii na kisiasa. Shirika hilo limeendelea kusema kuwa sheria ya kimataifa ya haki za binadamu, inalinda haki ya watu ya kutafuta, kupata na kutoa habari na maoni kupitia mifumo yote ya habari ikiwa ni pamoja na intaneti kwa njia huru.
Mashirika manne ya msaada yanayofanya shughuli zao katika maeneo yalioathirika, yameliambia shirika la Human Rights Watch kuwa shughuli zao zimetatizwa pakubwa kwasababu hayawezi kupokea habari muhimu kuhusu hali ya usalama na kibinadamu.Kwa mujibu wa afisa mmoja wa msaada, huduma za afya pia zimeathirika huku madaktari na wahudumu wa ambulansi wakishindwa kuwasiliana na wagonjwa.
Mnamo mwezi Agosti, Abiy aliwaambia wanahabari kwamba atakatiza kabisa huduma za intaneti iwapo vurugu zilizopsababisha mauaji zilizochowa kupitia mitandao ya kijamii zingeendelea na kusema kuwa huduma za intaneti sio maji au hewa hivyo basi sio muhimu.
Shirika la Human Rights Watch limesema kuwa badala ya kukatizwa kwa huduma hizo kwa ujumla na kuyazuia maandamano ya amani, serikali ya Ethiopia inapaswa kutumia vyombo vya habari kutoa habari wazi ambazo huenda zikapunguza ghasia na kuagiza vikosi vya usalama kuzingatia viwango vya kimataifa vya haki za binadamu.