1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaEthiopia

HRW: Wakimbizi wa Sudan wako hatarini nchini Ethiopia

17 Oktoba 2024

Mapigano kati ya vikosi vya shirikisho vya Ethiopia na wanamgambo kaskazini magharibi mwa nchini humo yanawaweka katika hatari kubwa wakimbizi wa vita kutoka Sudan.

https://p.dw.com/p/4lvOo
HRW: Wakimbizi wa Sudan nchini Ethiopia wamekuwa wakidhalilishwa
HRW: Wakimbizi wa Sudan nchini Ethiopia wamekuwa wakidhalilishwaPicha: Nariman El-Mofty/AP/picture alliance

Haya yamesemwa na shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch, lenye makao yake huko New York, Marekani.

Naibu mkurugenzi wa Human Rights Watch barani Afrika Laetitia Bader amesema wakimbizi wa Sudan nchini Ethiopia wamekuwa wakidhalilishwa na makundi tofauti ya wanamgambo waliojihami kwa zaidi ya mwaka sasa.

Katika ripoti yake, shirika hilo limesema kwamba watu waliojihami wamefanya mauaji, uporaji, utekaji nyara na kudai kulipwa pesa ili kuwaachia huru, na kuwafanyisha wakimbizi kazi za lazima karibu na kambi mbili.

Shirika hilo limesema limetuma matokeo yake ya awali ya ripoti hiyo kwa shirika la kuwahudumia wakimbizi la Ethiopia lililokiri kwamba kambi ziko karibu na maeneo yenye machafuko ila ikadai kuna usalama wa kutosha.