1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali ya Kongo yashutumiwa kukandamiza wapinzani

Sylvia Mwehozi
22 Agosti 2023

Shirika la haki za binadamu la Human Rights Watch limesema katika ripoti yake kwamba mamlaka nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo zimewalenga viongozi wa vyama vya upinzani kuelekea uchaguzi mkuu wa Desemba.

https://p.dw.com/p/4VRf4
Moise Katumbi
Kiongozi wa chama cha upinzani cha Ensemble pour la République Moise KatumbiPicha: Nicolas Maeterlinck/BELGA/dpa/picture alliance

Ukandamizaji huo unafanyika katikati mwa mvutano mkubwa wa kisiasa kuelekea kampeni rasmi za uchaguzi wa rais zitakazoanza Novemba 19 katika uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika Desemba 20. Human Rights Watch imesema kuwa mamlaka za Kongo zina wajibu chini ya sheria za kikanda na kimataifa za haki za binadamu kuhakikisha haki na uhuru wa kujieleza, kukusanyika, mikutano ya amani na kutembea vinatimizwa. Shirika hilo limezitaka mamlaka za Kongo kukomesha ukamatwaji wa kiholela na kuheshimu kikamilifu mchakato mzima na haki ya watuhumiwa kushitakiwa.

Soma pia: Mazungumzo ya Rais Tshisekedi na wapinzani yakwama

Thomas Fessy ambaye ni mtafiti mwandamizi wa Human Rights Watch nchini Kongo amesema kwamba "serikali ya Kongo inapaswa kuhakikisha kwamba wagombea wa upinzani, wafuasi wake na Wakongo wote wanakuwa huru kueleza mitizamo yao na maandamano ya amani kuelekea uchaguzi wa Desemba".

Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo Moise Katumbi
Wafuasi wa mwanasiasa Katumbi wakiwa wamehudhuria mkutano wa kiongozi huyo Kinshasa.Picha: JOHN WESSELS/AFP

Shirika hilo limeeleza kuwa mnamo Mei 23, polisi ilizuia msafara wa kiongozi wa chama cha upinzani cha Ensemble pour la République Moise Katumbikuingia jimbo la Kongo centrale ambalo liko kusini mwa mji mkuu wa Kinshasa, ambako alikuwa amepanga kufanya mikutano kadha ya kisiasa. Maafisa wa polisi walizuia magari ya Katumbi na washirika wake kwa maagizo kutoka kwa gavana wa mkoa, Guy Bandu Ndungidi.

Tukio jingine ni la Mei 25, polisi waliwazuia wagombea wa upinzani Katumbi, Martin Fayulu, Delly Sesanga, Matata Ponyo, na wafuasi wao kukusanyika nje ya Tume huru ya taifa ya uchaguzi. Hapo awali mamlaka zilikuwa zimeamuru wapinzani kutokusanyika hapo kupinga kile walichokitaja kama "mchakato wa uchaguzi wenye machafuko. Polisi walitumia mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya watu hao na kuwapiga baadhi ya waandamanaji. Siku mbili baadaye, viongozi walipiga marufuku maandamano mengine ya upinzani katika mji wa kusini wa Lubumbashi, na polisi walifunga barabara ili kuzuia waandamanaji kukusanyika.

Mei 30, maafisa wa ujasusi wa kijeshi walimkamata mshauri mkuu wa Katumbi, Salomon Kalonda, kwenye uwanja wa ndege wa N'djili wa Kinshasa alipokuwa akipanda ndege na Katumbi na washirika wengine. Kalonda alizuiliwa katika makao makuu ya kijasusi ya kijeshi hadi Juni 10, kisha akahamishiwa katika gereza la kijeshi la Ndolo la Kinshasa.

Martin Fayulu atembelea DW Bonn
Mwanasiasa wa upinzani Martin Fayulu alipotembelea ofisi za DW BonnPicha: Dirke Köpp/DW

Wanachama wa kitengo cha kijeshi cha Republican Guard, kinachomlinda rais, walimkamata mgombea mwingine wa urais wa upinzani, Franck Diongo, huko Kinshasa Juni 20 wakimtuhumu kwa kupatikana na silaha kinyume cha sheria. Alizuiliwa katika makao makuu ya upelelezi wa kijeshi, kisha akahamishiwa katika gereza la kijeshi la Ndolo mnamo Julai 8. Mwanasiasa mwenye umri wa miaka 61 na aliyekuwa msemaji wa chama cha kisiasa cha Katumbi Chérubin Okende, alipatikana amekufa akiwa na majeraha ya risasi kwenye gari lake mjini Kinshasa mnamo Julai 13.

Human Rights Watch inasema kuwa ukandamizaji wa serikali pia umekuwa na athari kwa namna vyombo vya habari vinavyoripoti taarifa za vyama vya upinzani. Shirika la kutetea haki za waandishi wa habari nchini Kongo JED lilisema Julai 31 kwamba lilikuwa na wasiwasi mkubwa kuhusu "kuongezeka kwa vitendo vya kutovumiliana na unyanyasaji wa kimwili dhidi ya waandishi wa habari na wafuasi wa vyama vya kisiasa" wakati wa kuandika matukio ya kisiasa.

Rais Félix Tshisekedi, ambaye anawania muhula wa pili, ameonyesha dhamira ndogo ya kuleta usawa kwa vyama vyote vya kisiasa kulingana na Human Rights Watch.

Chanzo: HRW