HRW: Rwanda yalaumiwa kwa kukiua haki za binadamu
13 Julai 2017Wengi kati ya watu hao walituhumiwa kwa wizi wa mikungu ya ndizi, ng'ombe au hata pikipiki huku wengine wakishukiwa kuhusika na uingizaji wa mihadarati kama vile bangi kupitia mpaka wa Rwanda na Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo au makosa ya kutumia nyavu za kuvulia samaki zilizopigwa marufuku.
Ripoti hiyo ya shirika la kutetea haki za binadamu yenye kurasa 40 iliyopewa jina ''Wezi wote lazima wauwawe'' na ambayo inaelezea mauaji hayo katika eneo la kaskazini mwa Rwanda imetoa maelezo ya kina ambayo yanaonyesha jinsi wanajeshi, polisi na vikosi vingine vya usalama nchini Rwanda vinavyo tekeleza mauaji hayo na mara nyingine vikiwa vinasaidiwa na raia.
Kwa mujibu wa ripoti ya shirika la habari la AFP shirika la kutetea haki za binadamu katika ripoti yake limeeleza kwamba wanajeshi walifika nyumbani kwa Fulgence Rukundo katika kijiji kimoja huko kaskazini mwa Rwanda na kumtuhumu kuwa aliiba ng'ombe hivyo basi walinda usalama hao walimbebesha Rukundo mzoga wa ng'ombe huyo mabegani mwake na kumpeleka katika shamba la migomba na hatimae walimpiga risasi na kumuua. Ripoti hiyo ya haki za binadamu imeeleza pia Rukundo ni miongoni mwa watu waliodhulumiwa maisha yao kwani badala ya kuwakamata na kuwafungulia mashtaka vikosi vya usalama viliamua kuwauwa.
Ripoti hiyo pia imetaja kuhusu raia walivyowauwa watu wawili baada ya utawala wa serikali za mitaa kuonekana kuwa inaunga mkono kuwauwa wezi. Shirika la kutetea haki za binadamu limesema watuhumiwa hao waliuwawa kabla ya kufanyika jitihada za kupata ukweli iwapo watu hao walikuwa na hatia au la.
Shirika hilo limesema hakuna ushahidi kuwa watu hao walikuwa hatari kwa maisha ya watu wengine. Mauaji hayo yanakisiwa yalitendeka kati ya mwezi Julai mwaka uliopita wa 2016 na mwezi Machi mwaka huu. Vilevile mauaji hayo yanachukuliwa kama njia mojawapo ya kueneza taharuki miongoni mwa raia kwa ajili ya kuwatisha wapinzani wa serikali.
Daniel Bekele mkurugenzi wa kitengo cha utetezi barani Afrika katika shirika la kutetea haki za binadamu Human Rights Watch amesema kuua katika jina la kupambana na uhalifu mdogomdogo haikubaliki na wala kitendo hicho hakifwati sheria bali kinajenga mazingira ya woga miongoni mwa watu. Bekele ameitaka serikali ya Rwanda kusitisha mara moja vitendo vya mauaji na iwachukulie hatua za kisheria wale waliohusika na mauaji hayo.
Rwanda imekuwa inachukuliwa kuwa ni mfano bora barani Afrika kutokana na mafanikio katika uchumi wake, miundo mbinu yake na katika maswala ya usalama.
Mwandishi: Zainab Aziz/AFPE/HRW - DW
Mhariri: Iddi Ssessanga