HRW lasema makundi ya kujihami yawalenga raia Mali
3 Novemba 2023Hayo yamesemwa na shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu Human Rights Watch lililoyataja mauaji hayo kama uhalifu wa kivita.
Katika ripoti iliyoonekana na shirika la habari la Ufaransa AFP, Human Rights Watch imesema kundi lililo na mafungamano na Al-Qaeda la Support Group for Islam and Muslims GSIM lilihusika na vifo vya karibu watu 135.
Shirika hilo limelilaumu kundi la GSIM kwa mauaji ya Septemba 7 ya watu 120 yaliyotokea katika feri moja huko Timbuktu.
Shirika hilo limeongeza kwamba wanajeshi wa Mali na wapiganaji kutoka kundi la mamluki wa Urusi la Wagner waliwauwa raia 40 katika operesheni tatu tofauti kati ya Aprili na Septemba.
Watawala wa kijeshi wa Mali waliingia katika ushirikiano na Wagner baada ya majeshi ya Ufaransa kuondoka nchini humo mwaka jana.