1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

HWR: Jeshi la Myanmar latuhumiwa kuchoma moto vijiji kadhaa

26 Mei 2020

Takriban nyumba 200 na majengo mengine yalichomwa moto katika nchini Myanmar, taifa linalokumbwa na machafuko.

https://p.dw.com/p/3cnAf
Myanmar - Soldaten der Kachin Independence Armee patrollieren
Picha: picture-alliance/AP Photo/E. Htusan

Uharibifu huo unaalama zote za uhalifu uliofanywa siku zilizopita na jeshi la Myanmar, linaelezea shirika la kimataifa kutetea haki za binadamu, Human Rights Watch.

Kwa mujibu wa ripoti ya Human Rights Watch, iliyowanukuu mashahidi na picha za satelaiti, wakaazi wa kijiji cha LetKar mashariki mwa jimbo la Rakhine, kaskazini magharibi mwa nchi hiyo ambao ni kutoka kabila la Rakhine wafuasi wa dini ya Kibudha, walikihama baada ya kuchomwa moto kwa makaazi kadhaa Mei 16.

Toka Januari mwaka jana, jeshi la Myanmar limekabiliana mara kwa mara na jeshi la Arakan (AA) ambao ni wanamgambo wa msituni waliojiimarisha wanaoiwakilisha jamii ya wachache ya wafuasi wa dini ya Kibudha wa jimbo la Rakhine.

Vita hivyo vimesababisha maelfu ya watu kuuawa na kuwalazimisha wengini 150,000 kuyakimbia makaazi yao.

Wanamgambo wakanusha kufanya uharibifu 

Wanamgambo hao wa AA wamekanusha kukichoma moto kijiji cha LetKar, mjini Mrauk U, huku kila upande ukimtupia lawama mwenzake katika kile ambacho shirika la HRW linaelezea visa hivyo vinawezekana kuwa uhalifu wa kivita.

BG Pink Lady Food Photographer of the Year 2020 | K M Asad
Picha: K M Asad

''Kuchomwa moto kwa kijiji cha LetKar kunaonyesha alama zote za vitendo vya uhalifu vya jeshi la Mynmar kwenye vijiji vya wa Rohingya miaka ya hivi karibuni'', alisema Phil Robertson, naibu kiongozi wa shirika la HRW kwa ajili ya bara la Asia.

Shirika hilo la kimataifa la kutetea haki za binadamu limetoa wito wa kufanyika kwa uchunguzi wa haraka na wa haki ili kufahamu kilichotokea na kuwafikisha mbele ya vyombo vya kisheria wahusika na kuwalipa fidia wathirika.

Warohingya wapatao 750,000 walikimbilia Bangladesh wakitokea kwenye jimbo la Rakhine baada ya vikosi vya usalama vya Myanmar kuanzisha ukandamizaji mwaka 2017 ikiwa ni katika kujibu shambulizi lililofanywa na kundi la waasi wa Rohingya.

Myanmar ilishitakiwa kwa kuhusika na mauwaji ya kimbari kwenye mahakama ya Juu ya Umoja wa Mataifa. Robertson anasema kwamba serikali ya Myanmar inatakiwa kuomba msaada wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya uchunguzi huo na sio kuliachia jeshi jukumu hilo.

Mwandishi : Saleh Mwanamilongo/AFP

Mhariri : Grace Patricia Kabogo