1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

HRW: China ni kitisho kikubwa kwa haki za binadamu

15 Januari 2020

Shirika la kutetea haki za binadamu lililo na makao yake New York Marekani Human Rights Watch, limesema China inaweka mikakati ya kuidhoofisha mifumo ya kulinda haki za binadamu kote duniani.

https://p.dw.com/p/3WDjG
Kenneth Roth Human Rights Watch
Picha: Getty Images/AFP/J. MacDougall

Shirika hilo limeyasema haya Jumatano katika uzinduzi wa ripoti yake ya kila mwaka baada ya mkurugenzi wake kuzuiliwa kuingia Hong Kong.

Mkurugenzi mtendaji wa Human Rights Watch Kenneth Roth katika taarifa amesema China imebuni mfumo wa upelelezi ambao ni wa kisasa kwa ajili ya kutazama na kuzuia ukosoaji wa umma.

Ripoti hiyo imezinduliwa mjini New York siku mbili baada ya Roth kukataliwa kuingia Hong Kong ambako alitazamiwa kuizindua ripoti hiyo wakati wa mkutano na waandishi wa habari. Kulingana na Wizara ya mambo ya nje ya China, Roth alizuiliwa kuingia kwa kuwa shirika la Human Rights Watch linaunga mkono maandamano ya kupigania demokrasia yanayoendelea Hong Kong. 

Kipindi kibaya zaidi cha ukandamizaji wa haki China

Ripoti hiyo imelaani wanayotendewa Waislamu katika eneo la Xinjiang nchini China.

"Hiki ndicho kipindi kibaya zaidi cha ukandamizaji katika miongo kadhaa ambacho tumekishuhudia China kutokea kipindi cha mapinduzi ya kitamaduni. Hali ni mbaya zaidi Xinjiang ambako Waislamu wa Uighur milioni moja au zaidi wanazuiliwa ili kuwawekea shinikizo la kuukataa Uislamu na tamaduni zao na hata lugha yao," alisema Roth.

Hongkong Proteste wg Uiguren
Polisi wakikabiliana na waandamanaji Hong KongPicha: AFP/A. Wallace

Human Rights Watch pia limeona kuwa serikali ya China chini ya Rais Xi Jinping inachukulia uanaharakati wa haki za binadamu nchini humo na miradi inayohusika na masuala hayo pamoja na sheria za kimataifa na taasisi zinazotetea haki kama kitisho.

Shirika hilo linasema uongozi wa China unajaribu kudhibiti kukosolewa kwake katika nchi za nje, inajaribu pia kuipuuza mijadala kuhusu haki za binadamu katika mikutano ya kimataifa na inadhoofisha pia mifumo ya dunia ya haki.

China iliiwekea vikwazo Human Rights Watch

"Kwa muda mrefu China imewanyamazisha wakosoaji wake nyumbani na kwa sasa serikali inajaribu kuwanyamazisha wakosoaji kote duniani pia," alisema Roth.

China Uiguren in der Provinz Xinjiang
Waislamu wa Uighur huko Xinjiang, ChinaPicha: AFP/G. Baker

Mwezi uliopita China ilitangaza vikwazo dhidi ya Human Rights Watch na mashirika mengine ya Marekani yasiyo ya kiserikali kama jawabu la sheria ya Marekani ya haki za binadamu na demokrasia kuhusu Hong Kong, ambayo inaunga mkono maandamano yanayoendelea huko na inatishia kuiwekea vikwazo China kutokana na ukiukaji wa haki za binadamu.

Katika uzinduzi wa ripoti hiyo, mwanadiplomasia wa China kwa Umoja wa Mataifa amemkosoa Roth kwa kusema ripoti hiyo imejaa uvumi na chuki na kuongeza kwamba China inayakataa yaliyomo kwenye ripoti hiyo. Amedai kwamba ripoti hiyo haijataja kwamba China imewatoa watu milioni 700 kutoka kwenye umaskini.