HRW: Baraza la Usalama liendelee kuichunguza Burundi
9 Desemba 2020Mnamo tarehe 4 Disemba, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa chini ya urais wa Afrika Kusini liliamuwa kusimamisha utolewaji wa taarifa mahsusi kuhusu Burundi na badala yake kuendelea na kuzungumzia masuala ya Burundi kwenye mikutano yake na mataifa ya Maziwa Makuu na Afrika ya Kati. Pamoja na kushikilia urais wa Baraza la Usalama, Afrika Kusini ndiyo pia mwenyekiti wa Umoja wa Afrika.
Lakini mkurugenzi wa Umoja wa Mataifa kwenye shirika la Human Rights Watch, Louis Charbonneau, amesema kwamba mikutano ya Baraza la Usalama juu ya Burundi imekuwa ikikosa umakini na muendelezo, huku Burundi na washirika wake wakijaribu kuzuwia uchunguzi juu ya hali ya nchi hiyo.
"Kiuhalisi ni kuwa ile hali ya ufuatiliaji wenye mipaka wa Baraza la Usalama kwa Burundi inaweza kuendelea kama ilivyokuwa awali, lakini kwa raia wengi wa Burundi, hatua hiyo inatuma ujumbe unaoogofya," alisema mkurugenzi huyo kwenye ripoti iliyotolewa leo (Disemba 9).
Matukio yanayohusu uvunjwaji wa haki za binaadamu na mauaji, kupotea kwa watu, na kuwekwa vizuizini yameshamiri nchini Burundi, licha ya matumaini ya mageuzi baada ya kuchaguliwa rais mpya mwezi Mei mwaka huu, kwa mujibu wa Human Rights Watch.
Burundi haitaki kufuatiliwa
Azimio Nambari 2303 lililopitishwa Julai 2016 na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilimtaka katibu mkuu wa umoja huo kuwasilisha ripoti mbele ya baraza juu ya hali ya Burundi kila baada ya miezi mitatu. Lakini serikali ya Burundi imekuwa tangu wakati huo ikiomba kila mara kuondolewa kwenye ajenda ya Baraza la Usalama.
Matokeo yake, mikutano ya kutowa ripoti imekuwa ikifanyika shaghala baghala na mara kadhaa iliahirishwa ama kufutwa kuelekea uchaguzi mkuu wa Mei mwaka huu nchini Burundi.
Sababu iliyokuwa ikitajwa na nchi hiyo kutishia kukata mawasiliano na Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Burundi, Michel Kafando, ambaye alijiuzulu Oktoba 2019 baada ya kutafautiana na serikali ya Burundi. Hadi sasa nafasi ya Kafando haijachukuliwa na mtu mwengine na ofisi yake imepangiwa kufungwa ifikapo mwezi Disemba 2021.
Lakini mkurugenzi wa Umoja wa Mataifa kwenye shirika la Human Rights Watch, Louis Charbonneau, anahoji kwamba "kuiwacha Burundi bila kuifuatilia ni kuruhusu na kubariki hali ya kutoheshimu sheria na haki za binaadamu, kinyume kabisa na dhamira ya kuasisiwa kwa Umoja wa Mataifa."