1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hezbollah wapata pigo uchaguzi wa Bunge Lebanon

17 Mei 2022

Vuguvugu la Hezbollah la Lebanon na washirika wake wanaounga mkono harakati za kundi hilo wamepata pigo baada kupoteza wingi wa viti bungeni katika uchaguzi uliofanyika siku ya Jumapili nchini humo.

https://p.dw.com/p/4BPcZ
Libanon I Wahlen
Picha: Joseph Eid/AFP/Getty Images

Hezbollah na washirika wake wamekuwa wakidhibiti wingi wa viti katika bunge la Lebanon tangu mwaka 2018.

Lakini uchaguzi uliofanyika siku ya Jumapili unaonesha kuwaendea kombo baada ya matokeo ya mwisho kuonesha vuguvugu hilo la kiislamu la madhehubu ya kishia limeshindwa kutetea idadi ya viti vingi bungeni.

Hezbollah na washirika wake wameambulia viti 61 badala ya 65 vinavyohitajika kuwa na wingi ya wabunge katika bunge la Lebanon lenye viti 128. Katika bunge linalomaliza muda wake vuguvUgu la Hezbollah na washirika wake walikuwa na viti 71.

Matokeo hayo ni pigo kubwa kwa Hezbollah na tawi lake la wapiganaji wanaomini kwamba mbali ya siasa za majukwaa njia za kutumia nguvu zinahitajika pia kuiimarisha Lebanon.

Washirika wa Hezbollah ndiyo chanzo cha anguko

Katika uchaguzi huo wagombea karibu wote wa Hezbollah, vuguvugu linalozingatiwa kuwa kundi la kigaidi na mataifa mengi ya magharibi wametetea viti vyao.

Libanon | Wahlen
Bango likiwaonesha viongozi wa Hezbollah kabla ya uchaguzi wa Jumapili Picha: Mohammed Zaatari/AP Photo/picture alliance

Lakini ni washirika wao wa chama cha Free Patriotic Movement cha rais  Michel Aoun ndiyo kimeangukia pua na kubadili mkondo wa kisiasa nchini Lebanon. Chama hicho kimeambulia viti 17 badala ya 20 ilivyokuwa ikidhibiti kabla ya uchaguzi.

Walionufaika kwa anguko hilo ni chama cha kikristo cha Christian Lebanese Forces CLF kinachoongozwa na mwanasiasa Samir Geagea, moja ya wakosoaji wakubwa wa kundi la Hezbollah na Iran, taifa linaounga mkono vuguvugu hilo la kisiasa.

Wenyewe wamenyakua viti 19 na kukifanya kuwa cha pili kwa wingi wa viti katika bunge la Lebanon. Wengine waliopata ushindi ni kundi la Druze linaloongozwa na Walid Joumblatt, wao wamejizolea viti vyote 8 vya bunge walivyokuwa wakiwania.

Hata hivyo washirika wengine wa Hezbollah, kundi la Amal la spika wa bunge Nabih Berri wamefanya vizuri kwa kupata ushindi wa viti vyote 27 vilivyotengwa mahsusi kwa makundi ya washia nchini Lebanon.

Wagombea binafsi na wanaharakati washinda viti vya Bunge 

Libanon I Wahlen
Uchaguzi huo umeshuhudia idadi ndogo ya wapiga kura Picha: Aziz Taher/REUTERS

Uchaguzi huo umeshuhudia pia wagombea binafsi na wanasiasa wageni ikiwemo wale wa vuguvugu la maandamano ya umma yaliyoitikisa Lebanon mwaka 2019 wakileta kishindo kikubwa kwa kunyakua viti 14 katika bunge linalokuja.

Kazi kubwa itakuwa ni kuunda serikali mpya, kumpata spika wa bunge na kumchagua rais mpya wa taifa hilo. Kwa kukosekana chama au muungano wenye wingi wa viti bungeni kutasadifu kuwa kizingiti kikubwa kwenye mchakato huo.

Lebanon yenyewe bado imo kwenye hali mbaya ya kiuchumi na iwapo mzozo mpya wa kisiasa wa kuunda serikali utaibuka, hilo litaongeza chumvi kwenye kidonda.

Licha ya ukweli kwamba Hezbollah na washirika wake wamepata pigo kwenye uchaguzi huo wa Jumapili, wachambuzi wengi wa siasa za Lebanon wanaamini hilo halitaleta mageuzi yote mapana kwenye taifa hilo dogo la Mashariki ya Kati.