Hatma ya Syria katika Jumuiya ya nchi za kiarabu kujadiliwa
5 Mei 2023Wanadiplomasia kutoka nchi za Kiarabu wanapanga kufanya kikao cha dharura mjini Cairo siku ya Jumapili kujadili kuhusu vita vinavyoendelea nchini Sudan pamoja na hatuwa za uwezekano wa Syria kurudishwa kwenye Jumuiya ya nchi za Kiarabu.
Ni zaidi ya mwongo mmoja tangu Syria iliposimamishwa uwanachama katika Jumuiya ya nchi za Kiarabu. Msemaji wa jumuiya hiyo Gamal Rushdy amethibitisha kwamba utafanyika mkutano Jumapili ambao unakuja katika wakati ambapo nchi za Kiarabu ikiwemo Misri na Saudi Arabia zimeanzisha mahusiano na rais Bashar al Assad na mawaziri wao wa mambo ya nje katika wiki za hivi karibuni walikwenda mjini Damascus.
Waziri wa mambo ya nje wa Syria nae pia alikwenda Cairo na baadae Riyadh mnamo mwezi wa Aprili ambayo ilikuwa ziara ya kwanza kwa kiongozi huyo kwa zaidi ya muongo mmoja. Syria ilisimamishwa kuwa mwanachama katika Jumuiya ya nchi za Kiarabu-Arab League yenye wanachama jumla 22 katika kipindi cha miezi ya mwanzo ya vita miaka 12 iliyopita na nchi za kiarabu baadae zikapitisha vikwazo vya kiuchumi dhidi ya nchi hiyo.
Vita nchini Syria vilisababisha vifo vya kiasi watu nusu milioni tangu mwezi Machi mwaka 2011 na nusu ya idadi ya wananchi wake milioni 23 kuachwa bila makaazi. Saudi Arabia inatarajiwa kuandaa mkutano wa kilele wa Jumuiya hiyo Mei 19 wakati suala la uanachama wa Syria kwa kiasi kikubwa linatarajiwa kuwekwa mezani.
Baadhi ya wanachama na hasa Qatar ambayo ina utajiri mkubwa wa nishati ya gesi zimepinga hatua ya Syria kurudishwa kwenye jumuiya hiyo. Novemba mwaka 2011 nchi 18 kati ya 22 za Jumuiya hiyo ziliunga mkono Syria kusimamishwa uanachama. Lebanon,Yemen na Syria yenyewe zilipiga kura ya kuupinga uamuzi huo wakati Iran ilijizuiwa kupiga kura.
Waziri wa mambo ya nje wa Jordan Ayman Safadi amekiambia kituo cha televisheni cha Marekani CNN kwamba anaamini kuna kura za kutosha miongoni mwa wanachama zitakazoisadia Syria kurudi kwenye Jumuiya hiyo.
Mkutano wa Jumapili mjini Cairo utajikita katika suala hilo la kuirudishia Syria uanachama na kikao hicho kinafanyika kwa ombi la Misri na Saudi Arabia kwa mujibu wa waziri wa mambo ya nje wa Jordan ambaye ni msemaji wa Jumuiya hiyo.
Mwanadiplomasia wa Iraq aliyezungumza na waandishi habari kwa sharti la kutotajwa jina kutokana na kutokuwa na mamlaka ya kuzungumza na waandishi amesema pamoja na mkutano huo kujadili suala la Syria na Sudan, pia utayatazama matukio ya hivi karibuni katika maeneo ya Israel na Palestina.