Hatimaye serikali ya mseto yatangazwa Israel
18 Mei 2020"Mimi, Benjamin Netanyahu, mtoto wa kiume wa Tzila na Benzion, kumbukumbu zao ziwe rehema, najitolea kama waziri mkuu na waziri mkuu mbadala kusalia kuwa mtiifu kwa taifa la Israel na sheria zake, kutimiza wajibu kwa imani kama waziri mkuu na waziri mkuu mbadala na kutekeleza maamuzi ya Knesset."
Alianza kuapishwa Netanyahu kisha akafuatilia Gantz.
"Mimi, Benjamin mtoto wa kiume wa Nachum na Malka Gantz, kumbukumbu zao ziwe rehema, najitolea kama waziri mkuu mbadala na kama waziri mkuu ajaye kusalia kuwa mtiifu kwa taifa la Israel na sheria zake, na kutimiza wajibu wangu kwa imani kama waziri mkuu mbadala na kutekeleza maamuzi ya Knesset."
Serikali hii inaundwa baada ya zaidi ya siku 500 za kutokuwa na serikali madhubuti na chaguzi tatu mfululizo.
Wajumbe wa bunge lenye viti 120 waliipigia kura serikali ya mseto itakayohudumu kwa miaka mitatu na kuuidhinisha kwa kura 73 za ndiyo dhidi ya 64 za hapana, huku mbunge mmoja akiwa hayupo bungeni.
Makubaliano ya kuunda serikali hii ya mseto yalifikiwa mwezi uliopita kati ya Netanyahu anayeelemea siasa kali za mrengo wa kulia na Gantz anayeelemea siasa za mrengo wa kati, mkuu wa zamani wa jeshi.
Awali, serikali hii ilikuwa itangazwe Alkhamis iliyopita, lakini Netanyahu akaomba siku nyengine tatu za kuamuwa juu ya nafasi za mawaziri wa chama chake cha siasa kali, Likud.
Changamoto kwa serikali mpya
Kwa makubaliano yao, Netanyahu atahudumu kwenye nafasi ya uwaziri mkuu kwa miezi 18, ambao ni ushindi mkubwa kwake hasa inapozingatiwa kesi ya ufisadi inayomkabili mahakamani. Gantz, kwa upande wake, atakuwa waziri mkuu mbadala, nafasi mpya kwenye serikali ya Israel, kwa nusu ya kwanza ya makubaliano yao. Kisha, ifikapo Novemba 17, 2021 watabadilishana nafasi.
Serikali hiyo mpya sasa inakabiliana na changamoto kubwa ndani ya zake za awali, ukiwemo uchumi uliosambaratishwa na janga la virusi vya korona na ahadi yake ya siku nyingi ya kuyanyakuwa maeneo makubwa ya Ukingo wa Magharibi.
Akizungumza kwenye bunge hilo kabla ya kura kupigwa, Netanyahu alisema wazi kwamba serikali itapaswa kuchukuwa mamlaka ya kulitawala eneo lenye makaazi ya walowezi ya Kiyahudi kwenye Ukingo wa Magharibi.
"Sasa ni wakati wa kutekeleza sheria ya Israel na kuandika ukurasa mwengine mtukufu kwenye historia ya Uzayuni," alisema Netanyahu.
Endapo itatekelezwa, hatua hiyo hapana shaka itazusha ukosowaji mkubwa wa kimataifa na kuchochea ghasia kwenye Ukingo wa Magharibi, ambako ni nyumbani kwa takribani Wapalestina milioni tatu na Waisraeli 400,000 wanaoishi kwenye makaazi yanayotambuliwa kuwa haramu kwa sheria za kimataifa.