1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

HARARE:Polisi yakanusha kumkamata tena Tsvangirai

29 Machi 2007
https://p.dw.com/p/CCEd

Polisi nchini Zimbabwe imekanusha taarifa kuwa imemkamata tena kiongozi wa chama kikuu cha Upinzani nchini humo cha MDC Morgan Tsvangirai.

Hata hivyo msemaji wa Polisi amesema kuwa wanachama 10 wa chama hicho wamekamatwa wakishukiwa kuhusika na ulipuaji wa mabomu ya petroli.

Lakini mashuhuda wanasema kuwa Tsvangirai alionekana akiingia katika makao makuu ya polisi mjini Harare, na haijafahamika wapi alipo.

Tukio hilo linatokea huku Rais Robert Mugabe akiwa mjini Dar es Salaam Tanzania kuhudhuria mkutano wa dharura wa wakuu wa nchi za Jumuiya ya Mandeleo ya Kusini mwa Afrika SADC.

Rais Mugabe aliwasili jana jioni mjini Dar es Salaam na kupewa ulinzi mkali ambapo pamoja na kuonekana kutaka kujibu maswali ya waandishi wa habari, walinzi wake na maafisa usalama wa Tanzania walimzuia.

Wakati huo huo wanaharakati kutoka Zimbabwe wapo mjini Dar es Salaam kutoa malalamiko yao kwa wakuu hao wa SADC.

Wanaharakati hao walimlaumu Rais Thabo Mbeki wa Afrika Kusini kwa kufumbia macho ukandamizaji unaofanywa na utawala wa Mugabe.