1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

HARARE: Tsvangirai kufikishwa mahakamani leo

13 Machi 2007
https://p.dw.com/p/CCJX

Kiongozi wa upinzani nchini Zimbabwe, Morgan Tsvangirai, anayesemekana alipigwa vibaya alipokuwa akizuiliwa na polisi, alitarajiwa kufikishwa mahakamani hii leo huku serikali ikiendelea kukosolewa kwa kuwashambulia waandamanaji wakati wa mkutano wa maombi uliofanyika juzi Jumapili mjini Harare.

Jaji Chinembiri Bhunu pia ameamuru Morgan Tsvangirai na Arthur Mutambara waruhusiwe kuonana na mawakili na madaktari wao baada ya serikali kukiri viongozi hao waliumizwa vibaya walipopigwa na polisi.

Hata hivyo mawakili wa Tsvangirai wansema polisi wanaomzuilia kiongozi huyo wamepuuza amri ya jaji huyo.

Jaji huyo aliamuru polisi wawafikishe mahakamani Tsvangirai, Mutambara na Lovemore Madhuku, mwenyekiti wa bunge la Zimbabwe kufikia saa sita mchana hii leo, la sivyo waachiliwe huru.

Akizungumza kuhusu kukamtwa kwa viongozi hao wa upinzani, msemaji wa upinzani nchini Zimbabwe, Jacob Mafume amesema kukamtwa kwao hakutazikwamisha juhudi zao.

´Kukamatwa kwa watu hawa kutazipeleka mbele ajenda za wananchi. Matakwa yetu ni ya haki na ni halali. Na mapambano yetu ya amani hayatakoma mpaka utawala mpya wenye uhuru, maendeleo na demokraisia utakapopatikana nchini Zimbabwe.´

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, ameilaumu serikali ya Zimbabwe na kutoa mwito viongozi hao wa upinzani waachiliwe huru na wahakikishiwe usalama.

Msemaji wa katibu mkuu huyo amesema mashambulio dhidi ya waandamanaji ni ukiukaji wa haki msingi ya raia kukutana kwa amani.