HARARE: Tsvangirai afikishwa mahakamani
13 Machi 2007Kiongozi wa upinzani nchini Zimbabwe, Morgan Tsvangirai, pamoja na wanaharakati wengine wa upinzani, wamefikishwa mahakamani hii leo kufuatia kukamatwa kwao mwishoni mwa juma lililopita.
Wafuasi wa upinzani na watetezi wengine waliimba nyimbo na kuonyesha ishara ya upinzani wakati kiongozi huyo pamoja na wengine sita walipotoka mahakamani.
Wakili wa Tsvangirai alisema hapo awali kwamba kiongozi huyo angebakia mahakamani kuungana na wafuasi wake lakini alilazimika kupelekwa hospitalini kwa matibabu.
Kiongozi huyo pamoja na wenzake walipigwa vibaya walipokuwa wakizuiliwa katika kituo cha polisi juzi Jumapili, baada ya kukamatwa wakati wa mkutano wa maombi mjini Harare.
Mbunge wa chama cha upinzani cha Movement for Democratic Change, Albert Nigel Bebe, amesema kukamatwa kwa viongozi wa upinzani nchini Zimbabwe kumechochewa kisiasa.
´Unaweza kuona mambo haya yote yamechochewa kisiasa na ni amri kutoka kwa serikali. Hawataki kusema wazi na kueleza ni kitu gani hasa kinachoendelea. Polisi hawajawafungulia mashtaka. Tumejaribu kuwasiliana na polisi na wametuahidi wanasubiri amri kutoka kwa viongozi wa vyeo vya juu.´
Hapo awali jaji Chinembiri Bhunu aliamuru polisi wawafikishe mahakamani Tsvangirai, Mutambara na Lovemore Madhuku, mwenyekiti wa bunge la Zimbabwe kufikia saa sita mchana hii leo, la sivyo waachiliwe huru.
Rais Robert Mugabe na serikali yake wamekosolewa vikali kwa kutiwa mbaroni viongozi hao wa upinzani. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, ameilaumu serikali ya Zimbabwe na kutoa mwito viongozi hao wa upinzani waachiliwe huru na wahakikishiwe usalama.